VIJANA WAHAMASISHWA KUWEKEZA KWENYE HISA KUJENGA UCHUMI IMARA WA BAADAYE

 



Na Woinde Shizza, Arusha


CRDB Bank Plc imewahamasisha vijana nchini kutumia fursa zilizopo katika soko la hisa na uchumi wa kidijitali kujijengea uhuru wa kifedha na mustakabali bora wa maisha yao.


Wito huo umetolewa jijini Arusha na Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB, Profesa Neema Mori, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa benki hiyo unaotarajiwa kufanyika Mei 15 na 16 mwaka huu.


Akizungumzia mkutano huo, Profesa Mori alisema kaulimbiu ya mwaka huu ya “Vijana na Uwekezaji katika Hisa” inalenga kuwajengea vijana uelewa wa uwekezaji na kuwahamasisha kushiriki katika masoko ya mitaji kama njia ya kujenga uchumi wa baadaye.


Alisema vijana wana nafasi kubwa ya kutumia teknolojia ya kidijitali, ubunifu na maarifa yao kuwekeza katika hisa na kuwa sehemu ya wamiliki wa taasisi kubwa za kifedha nchini.


“Ni wakati wa vijana kununua hisa na kuwa wawekezaji ili waweze kutumia ubunifu wa kidijitali kuonyesha vipaji vyao na kujikwamua kiuchumi,” alisema Profesa Mori.


Katika mkutano huo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Balozi Khamis Musa Omari huku wanahisa wakitarajiwa kujadili agenda mbalimbali ikiwemo ripoti ya mwaka, taarifa ya ukaguzi wa hesabu pamoja na uteuzi wa wajumbe wa bodi.


Profesa Mori alisema CRDB imependekeza gawio la shilingi 90 kwa kila hisa mwaka huu kutoka shilingi 65 za mwaka uliopita, hatua aliyoieleza kuwa ni matokeo ya ukuaji mkubwa wa benki hiyo na imani ya wanahisa wake.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Plc, Dk. Abdulmajid Nsekela, alisema mafanikio ya benki hiyo yametokana na ushirikiano mkubwa wa wanahisa, wateja na bodi ya wakurugenzi.


Alisema CRDB imeendelea kuimarika ndani na nje ya Tanzania kupitia falsafa ya diplomasia ya uchumi, jambo lililoifanya kuwa miongoni mwa taasisi imara za kifedha katika ukanda wa Afrika Mashariki.


“CRDB ni zaidi ya benki. Imevuka mipaka ya Tanzania na Afrika Mashariki kupitia falsafa ya diplomasia ya uchumi,” alisema Dk. Nsekela.


Aidha, alisema benki hiyo imeingia mwaka 2026 kwa mafanikio makubwa baada ya kupata faida baada ya kodi ya shilingi bilioni 206 katika robo ya kwanza ya mwaka huo.


Dk. Nsekela alisisitiza kuwa dhamira ya benki hiyo ni kuona vijana hawaishii kuwa wateja pekee, bali wanakuwa wawekezaji na sehemu ya nguvu ya uchumi wa taifa katika siku zijazo.



Naye Meneja wa CRDB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Sadat, alisema wanafarijika kuona mkutano huo ukifanyika Arusha kutokana na mchango mkubwa wa wateja wa kanda hiyo katika ukuaji wa benki.


Alisema huduma nyingi za kisasa na kidijitali zinazotolewa na CRDB Kanda ya Kaskazini zinasimamiwa na vijana wenye uelewa mkubwa wa teknolojia na ubunifu, hali inayochochea maendeleo ya huduma za kifedha nchini.



About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia