ARUSHA KUWAKA KESHO KATIKA SUBARU FESTIVAL 2026,




Na Woinde Shizza,Arusha

Jiji la Arusha linatarajiwa kuwa kitovu cha burudani na utalii kuanzia kesho Mei 15, 2026 hadi Mei 16, wakati wa kufanyika kwa tamasha kubwa la Subaru Festival 2026 litakalowakutanisha washiriki na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania katika viwanja vya Magereza jijini hapa.

Tamasha hilo litaanza kwa mkesha maalum utakaofanyika Mei 15 kabla ya kuendelea rasmi Mei 16 kwa shughuli mbalimbali za burudani, maonesho na hamasa ya utalii.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, muandaaji wa tamasha hilo Mercy Ntabago amesema lengo la festival hiyo ni kuitangaza Tanzania kimataifa pamoja na kuendelea kukuza sekta ya utalii kupitia matukio makubwa ya kijamii na burudani.

Aidha, Afisa Utamaduni wa Jiji la Arusha, Benson Maneno, amewataka waandaaji kutumia Subaru Festival kama jukwaa la kutangaza mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2027 jijini Arusha ili kuongeza hamasa kwa wananchi pamoja na wageni watakaotembelea mkoa huo.

Amesema matukio ya burudani yana nafasi kubwa katika kuitangaza Arusha na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia utalii na shughuli mbalimbali za kijamii.

Tamasha hilo linatarajiwa kuvutia washiriki kutoka maeneo mbalimbali duniani huku likitoa nafasi kwa jamii kushiriki katika shughuli za burudani, kuonesha vipaji na kukuza mshikamano wa kijamii.

Mbali na burudani, Subaru Festival 2026 pia inatajwa kuwa sehemu ya kuitangaza Arusha kama miongoni mwa miji inayoongoza kwa utalii na matukio makubwa nchini Tanzania.




About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia