DKT. HOMERA:SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MAGEUZI YA SEKTA YA SHERIA NCHINI
Na Woinde Shizza, Arusha
Waziri wa Katiba na Snheria, Juma Zuberi Homera amesema Serikali inaendelea kutekeleza maboresho mbalimbali yenye lengo la kuimarisha mageuzi katika Sekta ya Sheria nchini ili kwenda sambamba na mahitaji ya maendeleo ya taifa na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Homera ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo maalumu kwa Mawakili wa Serikali yaliyoandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, yanayofanyika jijini Arusha kuanzia Mei 18 hadi 20, 2026.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Mawakili wa Serikali wanapatiwa maarifa na ujuzi wa kisasa utakaoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Amesema mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo zimejikita katika maeneo ya kimkakati ikiwemo usimamizi wa mikataba ya ujenzi na manunuzi, sheria za anga na utatuzi wa migogoro ya anga, sheria za kodi katika sekta ya mafuta na gesi, uendeshaji wa mashauri ya kodi pamoja na mashauri katika mabaraza mbalimbali ya utoaji haki.
“Mada hizi ni muhimu katika kufanikisha maono ya mageuzi ya Sekta ya Sheria nchini na kuongeza uwezo wa Mawakili wa Serikali katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi,” amesema Dkt. Homera.
Aidha, Waziri huyo amesisitiza kuwa sheria ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na amani, utulivu na maendeleo ya kiuchumi, huku akibainisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka mkazo mkubwa katika misingi ya utawala bora, usalama, amani na utulivu.
Ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali wataweza kutoa ushauri sahihi wa kisheria, kusimamia mashauri ya Serikali kwa ufanisi na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine, Dkt. Homera amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuyafuatilia kwa umakini kutokana na umuhimu wa mada zinazojadiliwa katika kuboresha utendaji kazi wa sekta hiyo.
Kwa upande wake, Wakili Mkuu wa Serikali, Ally Possi amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali ili waweze kufanya kazi kwa viwango vya kitaifa na kimataifa.
Amesema mbali na kuongeza maarifa, mafunzo hayo yatawawezesha Mawakili wa Serikali kulinda rasilimali za taifa na kuongeza uwezo wa Serikali katika uratibu na uendeshaji wa mashauri mbalimbali yanayofunguliwa dhidi yake.
“Tunahitaji Jeshi la Kalamu lenye maarifa ya kisasa, uwezo wa kutumia mbinu za kidijitali katika usuluhishi wa migogoro pamoja na uwezo wa kuzuia migogoro kabla haijafika mahakamani,” amesema Dkt. Possi.
Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel M. Maneno amewahimiza Mawakili wa Serikali kuendelea kujifunza na kuongeza ujuzi ili kuendana na kasi ya uwekezaji na mabadiliko ya kiuchumi yanayoendelea nchini.
Amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria tayari zimeanza kutoa mafunzo maalumu kuhusu ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), ambapo zaidi ya mawakili 30 wamekwisha pata mafunzo na kuthibitishwa kuwa wataalamu katika eneo hilo.
“Lengo letu ni kuhakikisha miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi inasimamiwa kwa weledi mkubwa ili kuilinda Serikali na kuhakikisha taifa linapata wawekezaji wenye uwezo na viwango vya kimataifa,” amesema Mhe. Maneno.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kubadilika kimtazamo kwa Mawakili wa Serikali ili waweze kutoa ushauri wenye tija katika mikataba ya kimataifa na kuzuia migogoro isiyo ya lazima.
Ameongeza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga kuimarisha mfumo wa Preventive Legal Care kwa lengo la kupunguza mashauri mahakamani na kuiwezesha Serikali kuelekeza nguvu zaidi katika shughuli za maendeleo ya taifa.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanawakutanisha Mawakili wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali nchini na yanatarajiwa kuhitimishwa Mei 20, 2026 jijini Arusha






0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia