WANANCHI WAFURIKA UZINDUZI WA KAMBI YA MATIBABU BURE KALOLENI
.
Mamia ya wananchi wa jijini Arusha wamejitokeza kwa wingi katika Hospitali ya Wilaya ya Kaloleni kushiriki uzinduzi wa kambi maalum ya matibabu bure ya siku mbili inayofanyika hospitalini hapo, huku wakionesha mwitikio mkubwa wa kupata huduma mbalimbali za afya.
Uzinduzi wa kambi hiyo umefanywa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Dkt. Jacob Julius Rombo, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Arusha. Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wataalamu wa afya pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti ya jiji la Arusha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Rombo amesema serikali inaendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa karibu zaidi kupitia maboresho ya miundombinu ya afya na kampeni mbalimbali za utoaji huduma za matibabu.
Amesema kambi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha sekta ya afya na kuwafikishia wananchi huduma muhimu kwa urahisi.
Kwa upande wake, uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Kaloleni umeeleza kuwa wananchi watapata huduma mbalimbali bure ikiwemo uchunguzi wa afya, ushauri wa kitabibu pamoja na matibabu ya magonjwa tofauti katika kipindi chote cha siku mbili za kambi hiyo.
Wananchi waliojitokeza wamepongeza hatua hiyo wakisema itasaidia wengi kupata huduma ambazo wakati mwingine hushindwa kuzifikia kutokana na changamoto za kifedha.
About Woinde Shizza














0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia