BREAKING NEWS

Tuesday, June 21, 2011

EAST AFRICA CUP 2011 KUZINDULIWA LEO MOSHI

PILIKA za watu katikati ya mitaa ya Mji wa Moshi mkoani hapa zimeanza kuongezeka baada ya makundi ya washiriki wa tamasha la Michezo za Afrika Mashariki 2011 (East Africa Cup 2011) kuanza kuwasili mjini hapa.


Tamasha hilo ambalo linafanyika kwa mara ya tisa msimu huu limejumuisha vijana zaidi ya 1,300 kutoka nchi za Zambia, Kenya, Zimbabwe, Rwanda ,Uganda na wenyeji Tanzania bara na Zanzibar ambao kwa siku saba mfululizo watashiriki katika michezo mbalimbali itakayofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya Ufundi Moshi.

Taarifa iliyotolewa na Kamati ya Mashindano hayo kwa vyombo vya habari ilisema tamasha linafunguliwa rasmi leo(kesho)na Mkurugenzi wa Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Leonard Tadeo ambaye pia ataambatana na Naibu Mkurugenzi wa Michezo Diriani Yasoda.

Katika mashindano hayo vijana washiriki watapata fursa ya kushiriki kwenye mafunzo mbalimbali wakati wa asubuhi kabla ya michezo ambapo mada zitakazojadiliwa ni pamoja na Ukimwi na namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU, Huduma ya kwanza, Elimu ya Uongozi,Uamuzi na Utatuzi wa migogoro.


Akizungumzia tamasha hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, George Kamau alisema mashindano hayo ambayo yanafanyika Tanzania kwa mwaka wa nane mfululizo yanalenga kuwawezesha vijana kupitia michezo na kuongeza idadi ya vijana wa kike kushiriki ili kufikia uwiano wa usawa wa asilimia 50 kutoka wa sasa ambao ni asilimia 60 kwa 40.

“Mwaka huu idadi ya wanamichezo wa sichana imeongezeka kwakuwa wasichana wameanza kujitokeza na kushiriki kwa wingi hali ambayo inazidi kuonekana kukua mwaka hadi mwaka ambapo vijana wenye umri chini ya miaka 16 nusu kati yao ni wasichana”,alisema.

“Naamini vijana wa kike watakuwa chachu ya kufikisha ujumbe kwa vijana wenzao wa kike kushiriki katika michezo ili kujipatia mafanikio kama ilivyokuwa kwa mkuu wa waamuzi wa mashindano hayo ambaye kwa sasa anakuwa mwanamke wa kwanza kuwa na beji ya CAF”,alibainisha Kamau.

Shughuli nyinge zitakazoambatana na tamasha hilo la michezo ni pamoja na kuwawezesha vijana kujenga mahusiano baina yao na wengine kutoka nchi mbalimbali,nyakati za jioni baada ya michezo ya viwanjani kutakuwepo na mashindano ya utamaduni ambapo vikundi vya ngoma,nyimbo na maigizo vitashindana.

“Mbali na michezo hiyo pia kutakuwepo na semina kwa waandishi wa habari wa Afrika mashariki ambao wanashiriki kuripoti taarifa za mashindano hayo na kuendeleza viongozi vijana wanaohitaji kujiendeleza katika taaluma ya habari”alisema Kamau.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates