Baadhi ya familia za Jamii ya kimasai wilaya ya Longido mkoa Arusha,zinadaiwa kutumia sherehe za ubatizo kukeketa watoto wadogo ili kukwepa kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
Watoto wengi wadogo chini ya miaka miwili wamebainika kufanyiwa ukatili wa kukeketwa katika baadhi ya vijiji Wilaya ya Longido.
Wakizungumza katika uzinduzi wa mradi wa kupaza sauti kupinga matukio ya ukeketaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto Wilaya ya Longido ambao unatekelezwa na Shirika la wanahabari la MAIPAC kwa ufadhili wa Shirika la Cultural Survival, viongozi wa Serikali na Halmashauri ya Longido walionya serikali kuendelea kuwachukulia hatua wanaokeketa watoto.
Afisa Maendeleo wa halmashauri ya wilaya ya Longido,Rashid Hussein alisema baada ya serikali kuimarisha msako wa wanaokeketa watoto mbinu mpya imeibuka kwa watoto kukeketwa kwa Siri katika sherehe za ubatizo.
“Tayari tumebaini hili na tumetoa maelekezo kwa viongozi kuanzia ngazi za kitongoji kufatilia na wakibaini ukeketaji kwenye sherehe za Ubatizo watupe taarifa mapema “amesema.
Amesema hata hivyo wamebaini kumekuwepo na tatizo la baadhi ya viongozi kumaliza kesi kwa mazungumzo vijijini na akaonua viongozi ambao watafumbia macho ukeketaji katika maeneo Yao serikali itawachukulia hatua.
Wanawake wazuiwa kula wakiwa na ujauzito
Katika haya nyingine mganga Mkuu wa Wilaya ya Longido, Dk Methew Majani amesema wamebaini wanawake kuwa dhaifu wanapofikishwa hospitali kujifungua kutokana na kutopewa chakula ili eti waje kujifungua watoto wadogo.
Dk Majani alisema kwa kuwa wanawake wamekeketwa na ili kusipate shida zaidi wanapofika hospitali kujifungua wanazuia vya vyakula jambo ambalo limekuwa likisababisha uzazi pingamizi jambo ambalo ni hatari kwa maisha Yao na watoto.
“Lakini kibaya zaidi wanacheleweshwa kufika vituo vya afya akina mama wajawazito hili jambo halifai kwani serikali ya Rais Samia Suluhi imejitahidi kujenga vituo vya afya na hospitali ili wanawake wapate huduma nzuri na mapema zaidi”amesema.
Amesema ukeketaji umekuwa ukisababisha Vifo vya akina mama na watoto kutokana na kutokwa damu nyingi lakini pia kukosa nguvu za kujifungua Salama.
Mkurugenzi wa Shirika la MAIPAC,Mussa Juma alisema mradi huo umekuja baada ya waandishi kufanya utafiti katika wilaya hiyo na kubaini licha ya kazi kubwa ya Serikali na halmashauri kupinga ukeketaji lakini bado watoto wadogo wabakeketwa.
“Tuliwatuma waandishi vijijini kwenda kufanya uchunguzi nanwalitupa taarifa ambayo tulitumia kutafuta wafadhili kupata fedha ya kutoa elimu zaidi ya Kupambana na ukeketaji napaza sauti na tunamshukuru Cultural Survival kutufadhili”alisema
Wahanga wa ukeketaji watoa ushuhuda
Merikinoi orkesyanye alitoa ushuhuda kuwa amekeketwa na amezaa watoto wanane lakini wakati akijifungua Mtoto wa nane alipata tatizo la festura kutokana na kufanyiwa ukeketaji.
“Tumepata hii Shida kutokana na ukeketaji na ninashukuru mganga huyu wa wilaya na wengine wamenisaidia Sasa nimeona na naomba wanawake wenzangu na wazee wa Mila tuache ukeketaji kwani no hatari kwa afya zetu na watoto “alisema.
Akitoa mafunzo ya athari za ukeketaji , Mary Laizer alisema ukeketaji alisema yeye amekeketwa na anachokifanya kuhakikisha watoto hawakeketwi na ameweza kuvusha Mtoto wake wa kike Rika bila kukeketwa.
Mary alisema ukeketaji una madhara makubwa ikiwepo kutokwa damu nyingi,kuondoka starehe na kubwa kueleza kupoteza maisha ya mama na Mtoto.
Mary akionesha aina mbalimbali za ukeketaji na madhara yake na kuwataka wanawake na wanaume kuungana kupiga vita ukeketaji.
Katika mradi huo wa MAIPAC kwa kushirikiana na wadau ikiwepo shirika la Tembo na halmashauri wanatarajiwa kufika vijiji mbalimbali kupinga ukeketaji na kuunda kamati za vijiji kupinga ukeketaji.