NMB waipiga tafu mashindano ya kimataifa ya Diplomatic Golf.




Na Woinde Shizza,Arusha



Benki ya NMB imefanikiwa kukabidhi udhamini wa vifaa vya michezo kwa ajili ya wachezaji 150 wanaotarajia kushiriki mashindano ya kimataifa ya Diplomatic Golf 2024.


Michuano hiyo inayotarajia kuanza kutimua vumbi kwa siku mbili kuanzia Septemba 21-22, 2024 katika viwanja vya Kili Golf vilivyoko Mkoani Arusha yana lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu.


Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Songea Mississippi (SOMI) na klabu mwenyeji ya Kili Golf, jumla ya mashimo 36 yataamua mshindi kutoka kwa washiriki wote 150 kutoka nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na wachezaji kutoka Dubai na Marekani.


Mratibu wa mashindano hayo, Reinfrida Rwezaura, amesema kuwa maandalizi yote kuelekea mashindano hayo ya msimu wa sita mwaka huu yamekamilika.



Amesema lengo kuu la mashindano hayo ni kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia vituo vya kulelea watoto yatima na kuwasaidia wale wenye uhitaji, ikiwa ni pamoja na kusaidia wasichana wajawazito kurudi shule.


Pia mashindano haya yanatoa jukwaa la wachezaji kuonyeshana makali yao katika mchezo wa Gofu kutoka mikoa na nchi mbalimbali, pia yanatoa fursa kuonyesha ujuzi wao na nidhamu ya michezo lakini pia ya yanachangia jitihada za nchi za kukuza utalii kupitia michezo.


Kwa upande wake Meneja wa benki ya NMB, Kanda ya Kaskazini Baraka Ladislaus amesema kuwa wamedhamini jezi hizo kwa ajili ya kuvaa wachezaji ikiwemo fulana, kofia na taulo maalum za kujifutia jasho.


Amesema lengo la Benki ya NMB, kutoa udhamini huo ni kutokana na kuvutiwa na malengo yake ya  kusaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu.


"Mbali na udhamini huu lakini Benki pia imepeleka timu kushiriki mashindano haya, kwa ajili ya kuchangamana na jamii lakini pia kuonyesha uwezo wetu kama NMB katika michezo"


Amesema kuwa wao kama Benki wanaendelea kutoa masuluhisho mbalimbali ya kifedha kwa ajili ya kusaidia jamii kutatua changamoto zao za shughuli za kiuchumi na kijamii pia.


Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post