NMB YATOA VIFAA TIBA KWA SERIKALI KWA AJILI YA KUSAIDIA HUDUMA ZA AFYA

 


Serikali imefanikiwa kupokea vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi milioni 6.5 kutoka kwa Benki ya NMB kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa.

Vifaa hivyo ni mashuka 100, viti mwendo (2) chuma za kutundikia dripu (5) pamoja na Vitanda na magodoro (8) ikiwemo vitanda vitano vya kulaza wagonjwa na vitatu vya kuwapumzisha kwa ajili ya vipimo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Wilayani Monduli, Mkuu wa Idara ya Huduma za Kibenki kwa Serikali na Ofisi ya Makao Makuu ndogo ya NMB-Dodoma, Vicky Bishubo amesema, lengo la msaada huo ni kurahisisha utoaji huduma za afya kwa wananchi wanaofika kutibiwa katika hospitali hiyo ya Wilaya.

“Ni desturi ya Benki yetu kujipambanua katika mambo ya kijamii, ndio maana tulivyopata barua ya maombi ya vifaa hivi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Monduli, tuliipa kipaumbele ya kuhakikisha tunafanikisha hitaji hili na leo tumekuja kukabidhi”

Amesema kuwa nia ya benki ya NMB ni kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwahudumia wananchi, ambapo mbali na gawio wanalotoa linaloelekezwa kwenye shughuli za maendeleo lakini pia wamekuwa wakitoa misaada mbali mbali.

“Kama Benki tuna vipaumbele katika misaada yetu hasa kwenye sekta muhimu za Afya, na Elimu lakini pia kutoa afueni kwa wanaokumbwa na majanga kama mafuriko, na moto lakini pia tuna kapeni ya utunzaji wa mazingira kupitia upandaji wa miti” amesema Bishubo.

Nae Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus amesema kuwa katika kuendelea kuwahudumia wananchi, Taasisi hiyo imeendelea kuwa wabunifu wa bidhaa zenye kutatua changamoto za kifedha kwa jamii ikiwemo mikopo ta riba nafuu.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga amewashukuru NMB kwa msaada huo na kuwataka uongozi wa Hospitali kuzitunza ili ziweze kudumu na kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mbali na hilo aliwataka wahudumu wa Hospitali hiyo kuhakikisha vitanda na mashuka yanakuwa masafi mda wote bila kubadilisha rangi yake halisi ili iweze kuvutia wananchi wanaofika kufuata huduma kujisikia vizuri wanapolalia.

“Tunataka wagonjwa wanaokuja kufata huduma hapa watamani kuumwa ili walale tu, lakini haya mashuka yakibadilika rangi yake halisi kutoka meupe na kuwa ya kahawia kiukweli haipendezi hata kidogo, naomba muwe wasafi dhidi ya mashuka haya” amesema KIswaga.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Monduli, George Kasibante amesema kuwa hospitali hiyo ya miaka 1970 imefanikiwa kupatiwa zaidi ya shilingi milioni 500 hivi karibuni ya kufanya ukarabati na kujenga majengo matano ya kufulia, maabara, upasuaji na linalohudumia wagonjwa wa nje na la ofisi ya madaktari bingwa.

“Hali hiyo imeongeza wigo wa huduma kwa wagonjwa ikiwemo wa nje na wa kulazwa, sambamba na kuletwa kwa madaktari bingwa wa wamama, macho na meno imeondoa usumbufu wa wagonjwa kupatiwa rufaa za mara kwa mara kwenda Mount Meru jijini Arusha”


Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post