MMOJA AUAWA AKIJIANDAA KUFANYA UHALIFU


Jeshi la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kuzima tukio la uhalifu baada ya kumjeruhi kwa kumpiga risasi mtu mmoja anayesadikiwa kuwa ni jambazi wakati wakipambana na baadae kufariki dunia akiwa anapelekwa hospitali.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea jana Juni 04 eneo la Stand ya Hiace Kilombero muda wa saa 12:00 jioni, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) alisema kwamba jambazi huyo aliyejulikana kwa jina moja la Riziki anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 hadi 45 alikuwa anawasubiri wenzake ili wakavamie kituo kimoja wapo cha kuuzia mafuta kilichopo jijini hapa.

Alisema Jeshi la Polisi lilipata taarifa fiche juu ya uwepo wa jambazi huyo katika eneo hilo, ndipo askari walikwenda kwa nia ya kumkamata lakini mara baada ya kuwagundua alitoa bastola yake aina ya Chinese ambaye ilikuwa kiunoni na kuanza kushambulia kwa risasi.

“Wakati akiendelea kushambulia, risasi moja ilimjeruhi mpita njia aliyejulikana kwa jina la Halima Salim (20) Mkazi wa Arusha kwenye mguu wake wa kulia”. Alifafanua Kamanda Ng’anzi.

Kamanda Ng’anzi aliongeza kwa kusema “Mara baada ya askari kuona hali hiyo waliamua kujibu mapigo ambapo walimpiga risasi ambayo ilimjeruhi juu ya tumbo lake na kufariki dunia akiwa anapelekwa hospitali”. 

Kamanda Ng’anzi alisema, katika eneo la tukio wamekuta  silaha hiyo pamoja na risasi tatu kwenye magazine na maganda mawili ya risasi.

Aidha Kamanda Ng’anzi alitumia nafasi hiyo kuwaonya wahalifu kwa kuwaeleza kwamba jeshi hilo lipo macho na pia aliwaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano.

About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia