
Vijana halmashauri ya Arusha wameamua
kujikita, kwenye shughuli za ujasiriamali ili kupambana na hali ngumu ya
maisha inayowakabili, kutokana na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira
iliyowakumba vijana wengi kwa sasa.
Kufuatia changamoto hiyo, jumla ya
vijana 70 wenye nia ya kuwa wajasiriamali, kutoka kata 27 za halmashauri
ya Arusha, wametakiwa kuwa na malengo, yanaotekelezeka huku wakijikita
zaidi, kuangalia fursa na mahitaji ya jamii inayowazunguka katika
maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa na Meneja wa mradi
kutoka Asasi isiyo ya kiserikali ya Vissio For Youth, Vedastus Sigula,
wakati akitoa mafunzo ya siku moja kwa vijana hao, yaliyofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano, halmashauri ya Arusha.
Meneja huyo amefafanua kuwa ili kuwa
mjasiriamali ni lazima kuwa na malengo yanayotekelezeka na baada ya
malengo ni kuzitazama fursa ndipo una wazo la biashara.
"Jambo la kwanza kwa mjasiriamali ni
kuwa na lengo linalotekelezeka, pili angalia fursa zinazokuzunguka
kwenye eneo lako ndipo utoke na wazo la shughuli unayotaka kufanya, hapo
unaweza kufanikiwa" amesema Sigula.
Hata hivyo vijana hao, baada ya kupata
mafunzo hayo wameonyesha kupata mwanga juu ya ujasiriamali tofauti na
mawazo waliyokuwa nayo kabla ya mafunzo.
Stela Lomayani wa kijana wa kata ya
Mwandeti, amesema kuwa hakufahamu kama ujasiriamali una misingi yake ya
kufuata huku akijipambambanua kuwa sasa ana uwezo wa kuweka malengo,
kuchagua fursa, kuandaa andiko la mradi pamoja na kuweka mipango ya
kusimamia mradi huo.
"Nimejifunza namna ya kuweka malengo, si
malengo tuu, malengo yanayotekelezeka, kupambanua fursa, kutengeneza
business plan, jinsi ya kusimamia mradi kwa kuweka records za biashara"
amesema Stella.
Naye Elipokea Ayo kijana kutoka kijiji
cha Oldonyowas amethibitisha kutambua, jinsi ya kuanzisha biashara
inayoendana na mazingira na wakati husika huku akiwataka vijana wenzie
kutokukata tamaa kwa kukosa ajira badala yake kutumia fursa nyingi
zinazopatika katika maeneo yao.
Awali akifungua mafunzo hayo, Afisa
Maendeleo ya Jamii, halmashauri ya Arusha, Angela Mvaa, amewataka vijana
hao, kutumia fursa hiyo ya mafunzo kuwa na bidii katika kuendesha
biashara ili kupambana na changaomto ya ajira inayowakabili vijana
wengi kwa sasa.
Asasi ya Vission for Youth, imejipanga
kutoa mafunzo ya kibiashara kwa zaidi ya vijana 200 kwenye halmashauri
ya Jiji la Arusha na zile za wilaya ya Arumeru, kwa lengo la kuwapa
mbinu za ujasiriamali na kuwawezesha kuandika andiko la mradi, kwa
vijana watakao andika vizuri atapewa mkopo wa riba nafuu pamoja na
kusimamiwa mpaka vijana hao watakapokuwa na uwezo wa kusimamia biashara.