Ticker

6/recent/ticker-posts

KARATE YAGAWA MAENEO KWA WAFANYABIASHARA KUEPUSHA MIGOGORO



Na  Woinde  Shizza  ,Arusha.

Wilaya ya Karatu imegawa maeneo kwa Wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama Mama Ntilie na Wamachinga ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza kufuatia Wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao maeoneo yasiyo rasmi na kujikuta wakifukuzwa .

Mkuu wa Wilaya hiyo Bi.Theresia Mahongo amesema kuwa Wilaya hiyo imeamua kuwatengea maeoneo katika eneo la Mnadani ili kumaliza mgogoro uliokuwepo tangu mwaka 2000 baada ya Wafanyabiashara hao waliokua wakifanya biashara pembezoni mwa barabara kuondolewa ili kupisha ujenzi wa barabara ya Karatu /geti la Ngorongoro.

Bi.Theresia amesema kuwa wamewagawia maeoneo hayo ambayo wanaweza kujenga vibanda na kuweka mkataba na halmashauri juu ya ulipaji wa kodi ili waweze kufanya kazi zao bila kubughudhiwa na kujipatia kipato cha kila siku

Alisema kuwa jumla ya Wafanyabiashara 34 watagaiwa maeneo katika eneo la mnadani ambapo wanatarajia kulitumia eneo hilo katika biashara ndogo ndogo kwani wanatarajia kuwa eneo hilo litaendelezwa na kuwa na mzunguko mkubwa wa biashara.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Waziri Mourice amesema kuwa wataandaa mikataba ambayo itawasilisha maslahi ya pande zote mbili ,na kuongeza kuwa mpango huo unalenga kuwawezesha wananchi wanyonge kupata maeneo ya kufanya shughuli zao kama ilivyo serikali ya awamu ya tano ambayo imejipambanua kuwahudumia wananchi wanyonge.

“,Mpaka tarehe 15  mwezi huu tutakua tumeandaa mikataba baina ya halmashauri na wafanyabiashara ili waweze kuwa huru kujenga vibanda vyao na kuanza  ujenzi na kufanya shughuli zao” Alisema Mkurugenzi
Kwa Upande wao Wafanyabiashara hao  Evelina  Hando na  Fausta Saria wameishukuru serikali kwa kusikiliza kilio chao cha muda mrefu cha kuwapatia maeoneo ya kufanya shughuli zao kwani kwa muda mrefu walikua wakiteseka na kukosa maeoneo rasmi.

Evelina alisema kuwa wamekua wakiteseka tangu mwaka 2000  wamehamishwa mara kwa mara na kuibuka migogoro kati yao na wamiliki wa maeneo walipokuwa wanafanyia biashara lakini kwa sasa wanaishukuru serikali   kwa kuwapatia maeneo hayo.

Post a Comment

0 Comments