Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
Wito umetolewa unaowataka waislam wenye uwezo kiuchumi (vibopa) kutumia vyema sadaka zao kwa kuzitazama familia masikini katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.
Ushauri huo umetolewa na Mshauri wa Mufti mkuu wa baraza la waislam Tanzania (Bakwata) Sheikh Umar Yahya Ramia katika taarifa yake maalum ya kuukaribisha mwezi wa Ramadhan mjini Bagamoyo.
Sheikh Umar alisema miaka yote watu wenye uwezo kiuchumi wakijiitihidi sana kusaidia masikini na mafukara lakini akahimiza mwaka huu sadaka zao ziongezwe maradufu kwa kuzitazama familia duni.
Alisema itakuwa ni aibu na fedheha endapo kutakuwa na waislam ambao wana uwezo kiuchumi wakashindwa kuwasaidia watu masikini katika dhima ya kuwafanya waislam wengine washindwe kufunga kwa kukosa futari.
"Miaka yote kumekuwa na juhudi zinazifanywa na waislam wenye nguvu za kiuchumi wamizisaidia familia duni. Nashauri kwa dhati na yakin mwaka huu matajiri wawatazame zaidi masikini" Alisema sheikh Umar
Mshauri huyo wa Mufti na sheikh mkuu wa bakwata pia alisema kama ilivyo ada na kawaida ya waislam jambo la kukumbushana ni wajibu kwa njia ya heri hivyo akasema itapendeza wito huo ukazingatiwa na kutekelezwa kivitendo .
" Ramadhan ni mwezi wa heri kwa waumini kuchuma thawab . Ni mwezi mwema kwa watakaomtaka mungu msamaha .Atakaeongeza sadaka kwa masilini atasamehewa dhambi na makosa yake . Wenye uwezo wawasaidie masikini, wagonjwa, yatima na wajane "Alisisitiza.
Aidha alisema si jambo la busara ikiwa misaada itawaendea watu wenye unafuu wa maisha na kuwaachwa ambao hali zao kiuchumi ni duni na wengine wanafunga na kushindwa kupata futari.
"Majirani waalikane na kufuturu pamoja bila kuacha kufunga . Waislam wasaidiane ili kujenga upendo na udugu katika iimani .Mwezi huu watu waondoleane mifundo na vinyongo kwenye mioyo yao "alisema sheikh huyo
Sheikh Umar ambaye ni mjukuu wa Hayati sheikh Muhamad Ramia,aliwataka waumini wa kiislam popote walipo, wazinduke ili kuzidisha sala na dua, maombi na kutaka msamaha wa mungu .
"Ushauri wangu isiwe taklif kwa vibopa katika jamii .Haya ni mawazo yangu binafsi kwa nia njema kabisa .Awezae atimize wajibu huo na mungu hataacha kumlipa fadhila na thawabu Alielezea sheikh Umar
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia