Na Mwandishi wetu, Mirerani
MDAU wa maendeleo wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Taiko Kulunju Oletipa akiwa na marafiki zake ametembelea kituo cha watoto yatima na waliokuwa wanaishi kwenye mazingira magumu wa Light In Africa na kutoa msaada wa thamani ya shilingi milioni moja.
Taiko ametoa msaada huo ili kuwa faraja kwa watoto hao waone kwamba jamii bado inawajali hivyo wasihofie maisha katika hali wanayopitia.
"Tumetoa zawadi hii kwao ili kile ambacho tunakipata kwenye shughuli zetu tule kwa pamoja na watoto hawa ili nao wafurahi katika kituo hiki," amesema Taiko.
Ametoa wito kwa jamii na wadau wengine wa maendeleo kuwa na moyo wa kusaidia wahitaji kwa kile walichojaliwa na Mungu.
Hata hivyo, amewapongeza watumishi wa kituo cha Light In Africa kwa namna wanavyowahudumia na kuwasimamia watoto waliopo kwenye kituo hicho kwani wana siha njema na afya nzuri kimuonekano.
Ametoa msaada huo kwenye kituo hicho wa vyakula ikiwemo mchele, maharage, tambi, sukari, mafuta ya kupikia, majani ya chai, witta bixs, mafuta ya kujipaka, blue band, sabuni na pampas.
Ametoa msaada wa thamani ya shilingi milioni moja kwani vyakula hivyo ni vya thamani ya shilingi laki tano na kukabidhi fedha taslimu shilingi laki tano ili watoto hao waweze kujikimu.
Msimamizi wa kituo hicho, Mary Moria amemshukuru Taiko kwa kutoa msaada huo na kuahidi kuwa utatumika kama ulivyokusudiwa kwa watoto hao.
"Tunamshukuru Mungu kwa matoleo haya ambayo kwa namna moja au nyingine itawasaidia watoto hawa wakiwemo walemavu," amesema Mary.
Mdau mwingine, Sangari Leposo amesema wamemsindikiza Taiko ili kuwasalimia watoto hao na kuwatoa unyonge na wajihisi faraja katika maisha yao ya kila siku.
"Taiko ni mpenda maendeleo na mwenye moyo wa kusaidia wahitaji hivyo tumemsindikiza kwenye kituo hiki kumuunga mkono na pia watu wengine waige jambo hili jema," amesema Leposo.