RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya majumuisho ya ziara ya siku tatu mkoani Rukwa Julai 17, 2024 mbele ya maelfu ya wananchi wa Rukwa.
“Waziri Bashe nakuagiza nendeni na bei ya shilingi 700 ya mahindi. Na msimu ujao twende na ruzuku ya mbegu za mahindi na mbolea,” ameelekeza Mhe. Rais Dkt. Samia.
Katika ziara yake, amekagua na kuzindua pia miradi mbalimbali ya maendeleo na kuweka mawe ya msingi katika Sekta ya Afya, Elimu na Kilimo iliyopo Wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo.
Ameshukuru wakulima wa Rukwa kwa uzalishaji mzuri wa mazao na kuwaeleza kuwa uchumi wetu unaendelea kukua, huku miradi ya kimkakati inatekelezwa vizuri. Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yao ya Uwakilishi nao wamepongezwa kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguz ya Chama cha Mapinduzi.
“Niseme Rukwa inaruka na maendeleo. Uzalishaji unaendana na mahitaji,” amesema Mhe. Rais Dkt. Samia. Ameongeza kuwa ubora wa mazao unapimwa kwa kutumia teknolojia kuanzia kupima uzito wa mazao na hadi kwenye ubora wake.
Naye, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imehimizwa kuendelea kununua na kuhifadhi chakula kwa wingi ili nchi iweze pia kuuza nje ya nchi kibiashara. Amewahasa wananchi wanaouza kiholela mazao nje ya nchi kusitisha na kuhakikisha kuwa wanapata kibali cha kuuza mazao nje ya nchi kutoka Wizara ya Kilimo.
Tags
HABARI MATUKIO