WATU 57,607 wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wanatarajia kunufaika na maji baada ya mwenge wa uhuru kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji, unaotekelezwa na Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira jiji la Arusha (AUWSA).
Mkurugenzi mtendaji wa AUWSA Justin Rujomba akisoma taarifa ya mradi huo amesema matarajio ya mradi huo utakaozalisha lita 2,400,000 kwa siku ni kunufaisha watu 57,607 wa maeneo ya mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani na maeneo jirani ya kata za Shambarai na Naisinyai.
Rujomba amesema mradi huo unagharimu shilingi 4,373,838,884.62 fedha kutoka serikali kuu na hadi sasa shilingi 2,247,359,058.29 zimeshapokelewa na AUWSA na utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 75.
“Kazi zilizofanyika ni uchimbaji wa kisima kirefu, ujenzi wa nyumba ya mashine na uzio, kuvuta umeme, kufunga pampu ya kusukuma maji, kulaza bomba kuu kilomita 10.9 na bomba za kusambaza maji kilomita 48.6, ukarabati wa tenki la zamani lenye ujazo wa lita 150,00 kuunganisha maji kwa wateja 1,100 wa ndanin ya mji mdogo wa Mirerani na kuanza ujenzi wa tenki la lita 1,000,000’’ amesema.
Amesema mradi huo uliibuliwa mwaka 2020 baada ya serikali kubaini upungufu wa maji katika maeneo ya mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, hivyo serikali ikatoa maelekezo kwa AUWSA kufanya usanifu kwenye visima vilivyochimbwa kupitia mradi mkubwa wa maji jijini Arusha maeneo ya Valesca na Mbuguni kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji safi Mirerani.
“Ndugu kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 tunaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu, kwa heshima na taadhima tunaomba uukague na kuweka jiwe la msingi,” amesema Rujomba.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu wa 2024 Godfrey Eliakim Mnzava amewapongeza AUWSA kwa namna wanavyoendelea na ujenzi wa mradi huo na kuridhia kuweka jiwe la msingi.
"Ni matarajio makubwa ya jamii ya eneo hili kuwa mradi huu utakamilika kwa wakati na wao kupata huduma ya maji kwenye majumba yao na maeneo mengine zikiwemo taasisi mbalimbali," amesema Mnzava.
Mkazi wa kitongoji cha Kilimahewa kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani Saumu Bakari amesema kukamilika kwa mradi huo utafanikisha lengo la Rais Samia Suluhu Hassan la kumtua mama ndoo kichwani.
"Mradi ukikamilika na maji ya bomba yakivutwa majumbani kwetu, yatakuwa na manufaa makubwa kwa jamii hasa wanawake kwani wao ndiyo hutumia muda mwingi kufuata huduma ya maji umbali mrefu," amesema.