Mwandishi wetu.Babati
Taasisi ya Uhifadhi na Utalii ya Chem Chem Safaris, iliyopo eneo la hifadhi ya jamii ya wanyamapori ya Burunge(Buruge WMA), wilaya Babati Mkoa wa Manyara,imeshinda tuzo ya utalii na Uhifadhi unaoshirikisha jamii.
Tuzo hiyo, imetolewa na Taasisi ya kimataifa African Travel and Tourism Association(ATTA) ya nchini Uingereza, ambayo ilishirikisha nchi mbali mbali duniani.
Akitangaza ushindi wa chemchen Rais wa ATTA, Nigel Vere Nicoll, alisema walipokea idadi kubwa ya taasisi binafsi za Utalii na Uhifadhi, ambazo zinafanyakazi na jamii ili kupokea tuzo katika vipengere vinane ambavyo vinatambulika na shirikisho la Utalii duniani.
"Baada ya majaji kupitia sifa za kila taasisi na pia kupokea maoni kutoka kwa watalii waliotembelea maeneo hayo, Taasisi ya Chemchem ndio ilikuwa mshindi wa kwanza wa jumla kutokana na kuweza kushirikisha jamii katika eneo la Burunge WMA katika uhifadhi na Utalii na jamii kunufaika "alisema
Taasisi nyingine zilizotangazwa kushinda, katika utoaji wa tuzo hizo uliofanyika London uingereza ni kutoka nchi za Uingereza, Namibia, Kenya na Botswana.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Mkuu wa Taasisi ya Chem Chem, Clever Zullu alisema ushindi wa tuzo ya Uhifadhi na Utalii unaoshirikisha jamii, ambao wamepata umetokana na jitihada kubwa za Serikali na wadau wengine kukuza sekta ya utalii na uhifadhi nchini.
"Tunashukuru Chemchem kwa kupata tuzo hii ambayo ina maana kubwa sana katika shughuli zetu za Utalii na uhifadhi, ambao unashirikisha jamii kwa kiasi kikubwa"alisema
Zullu alisema ushindi huo ni matokeo pia ya kazi nzuri ya Rais Samia Suluhu kufungua nchi katika Utalii na kuvutia maelfu ya watalii duniani kuja Tanzania.
"Chem chem tutaendelea kushirikiana na serikali na taasisi za utalii na uhifadhi za TANAPA, TAWA, TAWIRI lakini pia Burunge WMA kuendeleza utalii na uhifadhi katika eneo hili kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo"alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa hotel ya chemchem, Elizabeth Omboi na mkuu wa Idara ya huduma mbali mbali katika hotel hiyo,Peter Corneli walisema ushindi huo, una maana kubwa kwao na utavutia watalii zaidi.
"Tumekuwa tukifanya shughuli za utalii wa hapa kwa kushirikisha jamii, tunatoa misaada kusaidia sekta za elimu, afya, mazingira na hata kusaidia makundi ya akina mama katika ujasiriamali"alisema Omboi.
Kwa upande wake, Corneli alisema miongoni mwa sababu nyingine ambazo zimekuwa zikivutia watalii kutembelea katika hoteli zao ni kupata chakula cha asili ya Kitanzania ambacho kimeandaliwa vizuri na kupata fursa ya kutembea kwa miguu katika maeneo ya wanyamapori ikiwepo kufika eneo la ziwa Manyara na kuona machweo na mawio ya jua.
Katibu Mkuu wa Burunge WMA, Benson Mwaise, alisema ushindi wa Chemchem ni ushindi wa Burunge WMA kwani, chem chem ni miongoni mwa taasisi ambazo zimewekeza katika eneo hilo.
"tumepata faraja kutokana na ushindi huu, dunia imetambua jitihada zetu katika uhifadhi lakini pia jamii inavyoshirikisha katika shughuli za Utalii na uhifadhi hili ni jambo kubwa sana"alisema
Taasisi nyingine ambazo zimepata tuzo hizo za hapa nchini ni Kisiwa cha chumbe kilichopo Zanzibar,Taasisi ya Asilia Afrika ya Uingereza, Lemala Camps and Lodges Tanzania.
Taasisi nyingine ni African Monarch Lodges ya Namibia,How Manyt Elephant ya Uingereza, Gamewatchers Safari&Porini Camp ya Kenya na Lets Go Travel Uniglobe ya Kenya.
Tuzo hiyo ya chemchem kama mshindi wa kwanza inatarajiwa kuwasilishwa nchini hivi karibuni na kushuhudiwa na serikali na wadau wa sekta ya utalii.