IMEELEZWA kuwa tafiti za kisayansi ili ziweze kuleta matokeo chanya kwa jamii ni muhimu zikapata nafasi ya kuandikwa kwenye vyombo vya habari .
Hayo yamesemwa leo Julai 17,2024 na Mkurugenzi wa ResearchCom Dr. Syriacus Buguzi , alipokuwa anazungumza na wadau wa afya ili kuwawezesha wanasayansi kuwasiliana kwa ufanisi kuelekea Kongamano la 11 la watafiti litakalofanyika Zanzibar.
"Research Com tumeingia ubia na Tanzania Health Summit ili kujenga kwa mazingira kwa watafiti na watu wanaoendesha miradi mbalimbali waweze kuwasilisha taarifa zao za kisanyansi zenye matokeo kwenye jamii jinisi ambavyo zinaweza kubadilisha maisha ya watu"
Amesema kuwa tafiti nyingi zinashindwa kuwasaidia wananchi kwa sababu ya kutowafikia.
"Kwa muda mrefu kumekuwepo changamoto kwa watafiti au wanayansi wanapofanya kazi zao hazipati nafasi katika vyombo vya habari kwa hivyo kunakuwa na changamoto kwao katika kuwasilisha hizi tafiti"
"Sisi tumetengeneza mazingira kwa wataalamu hawa kufanya kazi na waandishi wa habari ili zile kazi zao zipate nafasi ya kufahamika kwenye jamii na kutoa matokea chanya"
Akizungumza na Michuzi Blog, Nuru Ngailo Afisa mshauri wa mawasiliano na uchechemuaji katika Shirika la EGPAF amesema kuwa shirika hilo litatumia kongamano hilo kwa ajili ya kutoa elimu itakayowalenga vijana, Mama na mtoto juu ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na kifua kikuu.
"Kupitia mradi wa afya yangu unaofadhiliwa na watu wa Marekani USAID , tunatekeleza mradi huu Kanda ya Kati na Kaskazini mwa Tanzania..tumefikia watu wengi mathalani kule Singida tulimfikia mtu mmoja ambaye ni kiongozi katika jamii aliyekuwa anadhana ya kuwa mwanaume kupima HIV ni udhaifu lakini siku moja alipata kuusikia ujumbe wetu kupitia mhudumu wa afya tunayefanya naye kazi alielewa juu ya umuhimu wa kupima na sasa yeye amekuwa balozi wetu ana ameweza kuwafikia watu zaidi ya 900 kwa miezi sita tu tangu amejiunga. " Amesema
Amesema kuwa mradi huo umewafikia watu katika Mikoa sita nchini Tanziania ambapo wamekuwa wakikutana changamoto kubwa inayowakabili wanajamii ikiwa ni pamoja na tamaduni na mila potofu juu ya HIV .
"Changamoto kubwa ni watu kuwa na mila au tamaduni potofu kuhusiana na kupima HIV na Kifua Kikuu" amesema Nuru.
Amesema kuwa kwa upande wa Mama anayeishi na maambukizi ya HIV akiwa ana mtoto mdogo wanatoa elimu juu ya kumlinda mtoto kuanzia kipindi cha ujauzito mpaka anazaliwa ili mtoto azaliwe salama.
Akizungumzia juu ya takwimu za za wagonjwa tokea mradi huo ulipoanza Oktoba 2021 hadi Machi 2024, Meneja Mwandamizi na Ufuatiliaji wa Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) Frank Lyimo amesema mpaka sasa watu 1,608,798 walipimwa HIV ambapo kati yao watu 41,482 walikutwa wameathirika na watu 50,266 walinzishiwa matibabu.
Tags
HABARI MATUKIO