|
MWIGAMBA |
Jina
la ‘Maskini Mkulima’ lilijiunga na mtandao wa jamiiforums mnamo Desemba
27, 2011 na mpaka jana inaonyesha alikuwa ametuma zaidi ya Post 27
ikiwamo hii iliyokuwa na kicha cha habari: Wito kwa wana CHADEMA wote.
Makala
hiyo ambayo ndiyo imefanikisha kumbaini ilitumwa Jamiiforums Oktoba 19
Mwaka huu chini ya kichwa cha habari cha ‘Wito kwa wana CHADEMA wote!’,
inaeleza haya;
Kufuatia malumbano yanayoendelea kwenye vyombo vya
habari na madhaifu mengi ambayo tumeshayashuhudia kwenye chama kwa
sasa, natoa wito kwa wana CHADEMA wote nchini kwamba wakati umefika
tubadilishe uongozi wa juu wachama.
Kihistoria, CHADEMA kati
ya mwaka 2005 na 2010, agenda zetu kwa wananchi zilikuwa mbili. Kupiga
vita ufisadi, iliyosukumwa sana na Dr. Slaa na ile ya utetezi wa
raslimali zetu iliyobebwa na Zitto. Lakini sasa hivi chama kinaenda kwa
matukio.
Naandika nikiwa mwana CHADEMA safi na nataka kila
mwanachama atakayesoma atulie na kutafakari. Hili siyo jambo la
ushabiki. Nimawasiliano baina yetu wana chadema na tunahitaji tutulie na
kutafakari.
Nimekuwa
mwanachama wa siku nyingi na nimebahatika pia kuwa kiongozi ndani ya
chama kwa nyakati tofauti kwahiyo naelewa ninachokiandika.
Nadriki
kusema kwamba kwa sasa chama kinakwenda kwa matukio na ni bahati tu
kwamba CCM inaendelea kutupatia matukio lakini CCM na serikali yake
wakitunyima matukio, CHADEMA chini ya Mkt Mbowe, Katibu mkuu Slaa na
Naibu Zitto utakuwa ndo mwisho wake.
CHADEMA iliyopiga kelele
sana dhidi ya ufisadi, CHADEMA iliyopiga kelele mpaka sheria ya vyama
vya siasa ikabadilishwa na vyama kutakiwa kukaguliwa na Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), eti leo inaungana na CCM
kumshambulia mwenyekiti wakamati ya bunge ya hesabu za serikali (PAC)
kwa kutamka kwamba vyama havijawasilisha ripoti zake za fedha
zilizokaguliwa. Kwa nini? Muungano huu wa CHADEMA na CCM maana yake
nini?
Kama chama kinajiamini ni kisafi kwenye hesabu zake
hofu ni ya nini? Si wasubiri kikao na kamati ya bunge katibu mkuu aende
na hizo ripoti na nyaraka zinazoonyesha kweli wamewasilisha hesabu hizo?
Napenda
kabla sijaendelea mbele kuwapongeza wenyeviti wetu wawili wa kwanza
ambao kimsingi waliweka msingi mzuri sana wakutong’ang’ania madaraka na
badala yake kuachia mapema na kumwachia mwingine kidemokrasia bila
vurugu.
Hawakuwa madikteta na nawapongeza sana. Walijitahidi sana
kutokuwa wapenda madaraka na kimsingi walituwekea utamaduni ambao
walitaka wote tuufuate na kujenga taasisi imara inayojali demokrasia na
haki ya kila mwanachama.
Ni kwa msingi huo waliamua kuandika
kabisa katika katiba yetu kwamba kiongozi yeyote katika ngazi yoyote ya
kuchaguliwa atakapogombea na kushinda ataongoza kwa kipindi kimoja cha
miaka mitano na kisha ataweza kugombea nakuongoza kwa kipindi cha pili
cha miaka mitano baada ya hapo hawezi kugombea tena katika nafasi ile
ile aliyoitumikia kwa vipindi viwili.
Ili kuonyesha kwamba
walimaanisha kile walichokisema, wote wawili hawakuwahi kukaa madarakani
kwa vipindi viwili vilivyoruhusiwa katika katiba bali wote wawili
walikaa kipindi kimoja kimoja tu.
Napenda pia kumpongeza
mwenyekiti aliyepo madarakani, Mbowe. Kuna mengi kakifanyia chama.
Kakitoa kutoka kwenye chama cha tatu ama nne kwa upinzani hadi kuwa cha
kwanza na kustahili kuitwa chama kikuu cha upinzani.
Kakichukua kikiwa na wabunge 5 bungeni na leo katika kipindi chake cha miaka 10 kina wabunge 49.
Ni
achievement kubwa! Si hivyo tu, ni wakati wake CHADEMA imebeba agenda
nzito za kitaifa kama vile vita dhidi ya ufisadi, utetezi wa raslimali,
katiba mpya,nk.
Lakini kuna matatizo yameanza kujitokeza na
tusipochukua hatua haraka huko mbele tunaweza kupata shida kubwa. Ni
muhimu kwa Mbowe kuelewa kwamba uwezo wake umefikia hapo asitake
kulazimisha kusonga mbele akidhani bila yeye hakuna CHADEMA.
Akiache
chama kikiwa salama, abaki kama mwenyekiti mstaafu na awaachie wengine
awamu inayofuata ya kuingia madarakani. Kama hataki kuwa mwelewa na
kuachia ngazi, wanachama tumsaidie kwa kumpiga chini uchaguzi ujao.
Leo
nitaainisha mambo machache tu yanayohusiana na fedha za chama na
uaminifu ili wanachadema muelewe kwa nini viongozi wakuu wa chama
wamehamaki sana kusikia wanatakiwa kuwasilisha ripoti za fedha
wakajikuta wanapambana na mwenyekiti wa kamati ya bunge badala ya kamati
na hata kufikia kusahau kwamba huyo mwenyekiti wa kamati ya bunge ni
mwenzao, ni naibu katibu mkuu wa chama. Mengine nitaendelea kuyadondoa
siku nyingine nitakapopata fursa:
1. Wakati tukifanya
mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia
kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya
miaka mitano mitano.
Lakini wakati katiba inachapwa chini ya
uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela. Mambo
yanayotokea hivi leo yanaonyesha dhahiri kipengele hicho kiliondolewa
kwa makusudi kwa maslahi na kwa faida ya viongozi waliopo madarakani kwa
sasa.
Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo lakini kama
viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni
dhahiri hawawezi kuaminika na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa
nayenye athari zisizomithirika kwa chama.
Ni muhimu
wanachadema mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho
ndicho kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto
kupigania uenyekiti.
Kama kingekuwepo leo Mbowe alikuwa
anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo
kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi.
Ni
dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea
kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa akina Lyatonga
Mrema, John Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi kuuruhusu si kwa
Mbowe, bali kwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama
chetu.
2. Matumizi ya fedha za chama:
Hakuna mtu
anayejua hivi sasa fedha za chama zinatumikaje zaidi ya kakikundi ka
watu watatu yaani Mwenyekiti Taifa, katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha.
Maamuzi
ya vikao hayaheshimiki tena na mabwana hawa. Baada ya uchaguzi wa 2010
vikao halali vilielekeza kiasi na aina ya fedha ambazo hazitaguswa bali
zitunzwe kwenye akaunti maalum kwa ajili ya uchaguzi wa 2015. Lakini leo
si tu akaunti hiyo haina fedha bali hakuna akaunti yoyote yenye fedha.
Watu
watatu ndo wanaamua fedha zitumikeje. Mfano mwingine ni maamuzi ya
kikao cha Baraza kuu cha mwezi January kilichoamua kwamba kiasi cha
fedha inayotoka serikalini kipelekwe kwenye mikoa, wilaya namajimbo na
kiasi kingine kipelekwe kwenye kanda. Leo ni mwezi wa 10 maamuzi hayo
hayajatekelezwa ipasavyo.
Nyinyi viongozi wa kanda,mikoa,
wilaya na majimbo ni mashahidi wa hili . Lakini kuna michango ya watu
binafsi kama Mzee Sabodo, hizo nazo hazijulikani zimechukuliwa lini kwa
mfumo gani, zikatunzwa wapi na hatimaye zimetumikaje.
Hapo
sijataja fedha zinazopatikana kutoka kwenye fundraising events
mbalimbali kama ile ya Dar es Salaam na Mwanza. Hizo nazo hazijawahi
kuonekana na walioendesha hizo fundraising, uaminifu wao kwenye masuala
ya fedha ni questionable.
3. Taarifa za fedha
Tokea
baada ya uchaguzi wa 2010 mpaka leo, hakuna kikao chochote kilichowahi
kupokea na kujadili hadi mwisho ripoti ya mapato na matumizi ya fedha za
chama.
Kila kikao agenda hiyo inarushwa kiaina. Wanaojua mchezo huo
ni watu watatu tu niliowataja hapo juu na malengo ya kurusha hiyo agenda
kila wakati na kukwepesha isijadiliwe pia wanayajua wao.
Ni dhahiri
tukiendelea na hawa watu tutafika 2015 tukiwa hatuna pesa hata ya kuweka
mawakala kwenye vituo na tutapigwa tukiwa tumesimama.
4. Mipango ya kukipatia chama mapato ya ziada kutoka nje ya chama
Wakuu
waliopo hawana hata ndoto ya namna ya kupata fedha za ziada.
Wanachokijua ni kukusanya ‘sadaka’ kwenye mikutano ya hadhara na
kuwapatia kazi watu wanaoonekana kuwa matapeli eti waendeshe harambee za
kuchangisha fedha kwa njia ya matukio.
Mawazo mazuri kama la
kuanzisha kampuni la uwekezaji la chama litakalowekeza kwenye miradi
mbalimbali, halijawahi kufanyiwa kazi, na hivyo uanzishaji wa miradi
mbalimbali ya kuiingizia taasisi fedha imebaki ndoto ya mchana.
Hatuwezi
kufika hata siku moja bila fedha. Hata uchaguzi wa wenzetu wa Kenya
juzi juzi wakuu wetu ingawa walishiriki lakini hawaonekani kama
wamejifunza chochote.
5. Matumizi mabaya ya madaraka yanayoweza kuhusishwa na ufisadi
Chama
chetu kinayo kamati ya tenda ambayo iko chini ya sekretariat. Lakini
kamati hii haifanyi kazi imezimwa kimya kimya na wajumbe wote wa kamati
ya tenda kwa kuwa ni wachumia tumbo wanaojigonga kwa wakuu,wamekubali
kuzimwa.
Leo ikidaiwa kamati hiyo ilete nyaraka za mchakato wa
manunuzi ya magari, pikipiki, kadi za uanachama, set ya televisheni
iliyofungwa ofisini kwa katibu mkuu, hawana.
Manunuzi haya yote
yanafanywa na wakuu bila utaratibu wowote jambo ambalo ni hatari na
linarahisisha matendo ya kifisadi. Hivi tunavyoongea, ni mwenyekiti
taifa mwenyewe ndiye aliyenunua magari na pikipiki zote za M4C.
Hivi
tunavyoongea kuna shilingi milioni 80 ambazo mwenyekiti taifa
alizichukua na kuagiza kadi za uanachama tangu mwaka jana mpaka leo hizo
kadi hazijawahi kuonekana.
Na mwenyekiti anafanya mambo hayo
yote akitambua kwamba yeye ni mwenyekiti na hayo ni masuala ya
kiutendaji ambayo yako chini ya katibu mkuu kama mtendaji mkuu wa chama
na kamati yake ya tenda. Huu si ufisadi ni nini?
6. Makubaliano ya kifisadi na mtu binafsi anayeuza vifaa vya uenezi vya chama
Hakuna
kikao chochote cha juu kilichojadili ama kilichowahi hata kupewa
taarifa tu kwamba sasa kuna mtu binafsi kapewa tenda ya kuuza.
Mwenyekiti
wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Ndugu Samson Mwigamba amesimamishwa nafasi
ya uongozi mara moja kuanzia jana na Baraza la Uongozi la Kanda ya
Kaskazini, huku taratibu zingine za kinidhamu zikiendelea kwa kufuata
katiba, kanuni, maadili, miongozo na taratibu za chama.
Kikao
hicho kimechukua hatua hizo mara moja baada ya Ndugu Mwigamba kukiri
kwa maandishi kuwa ameandika kwa kutumia jina bandia na kutuma kwenye
mitandao ya kijamii, kutoa tuhuma za uongo na kupotosha umma dhidi ya
chama na viongozi, kinyume na katiba, kanuni, maadili, miongozo na
taratibu za chama.
Hatua hiyo ya kukiri na kusimamishwa uongozi,
ilifuatia baada ya Ndugu Mwigamba kutuhumiwa kusambaza katika mitandao
tuhuma za uongo, upotoshaji na uchonganishi, ambapo kikao kilimwagiza
kusalimisha kompyuta yake ili wataalam wa masuala ya IT wa CHADEMA,
Kanda ya Kaskazini, waweze kufanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo.
Wataalam
hao wa masuala ya IT, wakitumia ushahidi uliokuwa katika bandiko hilo,
hasa jina la kiongozi huyo, walibaini pasi na shaka kuwa andiko
lililosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, kwa kutumia jina bandia
liliandikwa na kuhifadhiwa kwenye kompyuta ya Mwigamba kisha kupostiwa
jana.
Ndugu Mwigamba
ametuhumiwa kusambaza andiko hilo akiwa katikati ya kikao, baada ya
amemaliza kuwasilisha taarifa ya hali ya chama katika mkoa wake wa
Arusha, ambapo alikisifia chama na uongozi wa taifa kwa kutekeleza
maagizo ya vikao vya chama na kubuni mipango na mikakati mbalimbali ya
kukiendesha chama ili kuiondoa CCM madarakani.
Kikao
hicho cha Baraza la Uongozi, chini ya uenyekiti wa Mh. Israel Natse,
Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini (Tanga, Manyara, Kilimanjaro na
Arusha), kiliazimia kwa kauli moja kumsimamisha Mwigamba, huku taratibu
zingine za kushughulikia masuala ya kinidhamu zikifuata
- See more at: http://wazalendo25.blogspot.com/2013/10/mwenyekiti-wa-chadema-arusha-samson.html#sthash.K7vxrkx7.dpuf
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia