Mwasisi wa Chadema Edwin Mtei (mwenye kofia) akizungumza kwenye
mkutano wa siku tatu wa Baraza la Kanda ya Kaskazini ya chama hicho
jijini Arusha juzi.Picha na Filbert Rweyemamu
Mkutano wa Baraza la Uongozi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Kanda ya Kaskazini juzi uligeuka ukumbi wa ngumi, baada ya
Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kushushiwa
kipigo.
Mwigamba alishushiwa kipigo hicho na baadhi ya viongozi wenzake wa
chama kwa madai ya usaliti na tayari amesimamishwa uongozi kwa muda
usiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas jana alithibitisha
kutokea kwa vurugu hizo na viongozi hao wa Chadema kufikishana polisi.
Alikutwa na zahama hiyo mbele ya viongozi wakuu wa Chadema Taifa,
Mwenyekiti, Freeman Mbowe na mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei katika
Hoteli ya Corridor Springs.
Viongozi hao wamekuwa wakifanya ziara za aina hiyo nchi nzima,
kuimarisha chama na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa
mwakani na uchaguzi mkuu ujao wa Rais na wabunge mwaka 2015.
Habari kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa hatua hiyo
ilifuatia tuhuma kwamba Mwigamba alituma ujumbe kwenye mtandao wa
kijamii wa Jamii Forums, unaodaiwa kukichafua chama hicho.
Tukio hilo la aina yake lilitokea wakati viongozi wote wa juu wa
chama hicho, wakiongozwa na Mbowe walipokuwa wakijadili mustakabali wa
chama hicho, mkutano ambao ulihudhuriwa na wabunge karibu wote wa
Chadema wa kanda hiyo.
Hata hivyo, wakati mijadala ikiendelea baadhi ya viongozi wa chama
hicho, akiwamo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema
walimtuhumu Mwigamba kutuma ujumbe kwenye mtandao huo, uliokuwa
ukizungumzia ufisadi ndani ya chama hicho, wakidai alitaka Mwenyekiti
Mbowe kukubali kuchunguzwa.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mwigamba alisema kuwa baada
ya Lema kutoa tuhuma hizo aliungwa mkono na viongozi wengine na vijana
waliokuwa wameimarisha ulinzi, kumvamia na kuanza kumpiga pamoja na
kumnyang'anya kwa nguvu kompyuta mpakato (Laptop), aliyokuwa nayo, kisha
kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi, mjini Arusha.
"Wamenipiga sana na kuniweka ndani, ila nashukuru Mkuu wa Upelelezi
wa Wilaya ya Arusha (OCCID), alikuja na kunitoa saa 5:00 asubuhi,"
alisema Mwigamba.
Alisema kuwa leo katika mkutano wake na waandishi wa habari ataeleza
yote yaliyotokea na hatua atakazochukua, kwa kuwa yeye ni kiongozi wa
juu wa chama.
Hata hivyo, alieleza kwamba bado anashauriana na wanasheria wake kuona kama anaweza kuwachukulia hatua waliompinga.
Kauli ya polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema polisi
wameona hakuna kosa la kisheria lililotokea hasa kutokana na malalamiko
yaliyofikishwa kwao dhidi ya Mwigamba ya kukichafua chama kwenye
mitandao.
"Hili suala la mitandao ni kubwa na lina taratibu zake sasa kusema tu
umechafuliwa na iwe kesi nadhani uchunguzi unahitajika kwao, sisi
tumeona haya ni mambo yao wanaweza kuyamaliza wao ndiyo sababu
tulimwachia, Mwigamba," alisema Sabas.
Kosa analodaiwa kufanya Mwigamba
Akizungumzia sakata hilo jana, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
alisema kwamba Mwigamba alibainika kutuma ujumbe kwenye mtandao wa Jamii
Forums uliokichafua chama hicho, akieleza haikuwa mara yake ya kwanza
kwa kiongozi huyo kufanya hivyo na kwamba walikuwa wakimfuatilia kwa
muda mrefu.
"Kilichotokea ni hicho, vijana wa Red Brigade ndio waliomtoa
ukumbini, baada ya kumbaini kukichafua chama, kwani laptop yake baada ya
kuchunguzwa na wataalamu wetu walijiridhisha ni yeye ndiye aliyetuma
ujumbe huo," alisema Lema.
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alitaja tuhuma
zinazomkabili Mwigamba kuwa ni pamoja na kusema uongo, kupotosha taarifa
za chama na kuchonganisha viongozi kupitia mtandao wa kijamii ya Jamii
Forums.
Katika andiko lake kwenye mtandao, Mwigamba anadaiwa kuwatuhumu
viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na
Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa kuwa wamechakachua katiba ya chama hicho
kuhusu ukomo wa nafasi za uongozi ili kujinufaisha binafsi.
Golugwa alisema kuwa baada ya kubanwa kwenye kikao, Mwigamba alikiri
kuandika na kurusha taarifa hizo kwenye mitandao, lakini alipotakiwa
kukabidhi kompyuta yake ili ichunguzwe na wataalamu wa mawasiliano wa
chama hicho aligoma, hali iliyozua tafrani kati yake na walinzi wa chama
hicho (Red Brigade), waliolazimika kutumia nguvu kumdhibiti.
Purukushani zilivyotokea
Habari zaidi zinaeleza kuwa katika harakati za kutaka kumnyang'anya
Mwigamba kompyuta yake, mwenyekiti huyo wa Chadema mkoani Arusha alianza
kushambuliwa na baadhi ya viongozi wa Chadema, kabla ya kufanikiwa
kumdhibiti.
Zinaeleza kuwa katika tukio hilo kulitokea pia kurushiana maneno na
matusi ya nguoni kati yake na viongozi wengine wa chama hicho akiwamo
Lema.
Baadaye Lema aliliambia gazeti hili kwamba katika purukushani hizo Mwigamba alimrushia ngumi ambayo hata hivyo aliikwepa.
Alisema kuwa wanakusudia kumfungulia kesi Mwigamba ya kukichafua chama chao katika mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, alisema kikao chao kiliendelea jana bila ya vurugu zozote
na kuweka mikakati ya kushinda majimbo yote ya Kanda ya Kaskazini mwaka
2015 na kuchukua nchi katika uchaguzi huo ujao.
Adhabu kwa Mwigamba
Katika hatua nyingine Chadema, kimemsimamisha uongozi Mwigamba kwa
tuhuma za kukisaliti, kukihujumu chama hicho na viongozi wake.
Akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha
jana, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel Natse alibainisha
kuwa uamuzi wa kumsimamisha Mwigamba katika nyadhifa zote za uongozi
ndani ya chama ulifikiwa na kikao cha Baraza la Uongozi wa Kanda ya
Kaskazini kilichokutana juzi.
Alisema kuwa Mwigamba amesimamishwa kwa muda usiojulikana kupisha
uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kuonya kuwa iwapo tuhuma
zitathibitishwa, hatua nyingine za kinidhamu zitafuata kulingana na
kanuni na katiba ya Chadema.
"Kwa sasa Mwigamba anatuhumiwa kuvunja sura ya kumi, kifungu cha 10.1
kifungu kidogo cha 8, 9 na 10 ya katiba ya Chadema inayozungumzia
maadili ya uongozi," alisema Natse.
Akifafanua zaidi alisema kuwa sura na vifungu hivyo vinakataza
kiongozi wa chama hicho kutoa tuhuma dhidi ya viongozi wenzake bila
kufuata vikao halali vya kikanuni na kikatiba.
HABARI kwa hisani ya rweyumamu info blog
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia