Ticker

6/recent/ticker-posts

DAR WALIHITAJI TAMASHA LA PASAKA

 
NA MWANDISHI WETU
 
WADAU wa muziki wa injili wa jijini Dar es Salaam wameingiwa na hofu juu ya Tamasha la Pasaka kama mwaka huu litafanyika ama litaishia mikoani kwa maraya kwanza katika historia yake tangu lianzishwe mwaka 2000.
Hofu ya wadau hao Tamasha hilo inatokana na hatua ya waratibu wake Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam kuitaja  mikoa ya Geita,Mwanza na  Shinyanga pekee, hivyo wapenzi na mashabiki wa jijini Dar es Salaam kuhoji kulikoni.
Akizungumza jana , Anastazia Ferdinand Malinza wa Machimbo, Temeke jijini Dar es Salaam, alisema ameshtushwa kuona waratibu wanataja tamasha hilo mikoani tu na kujiuliza kuna kitu gani kimetokea.
 “Kwa miaka mingi tumezoea liwe Tamasha la Pasaka au Krismasi, limekuwa likianzia jijini Dar es Salaam ndipo liende kwingineko mikoani kulingana na uwezo wa waratibu, lakini safari hii tunasikia tu Geita, Mwanza na Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga,” alisema Annastazia.
 Alisema akiwa mpenzi na shabiki wa tamasha hilo ambalo limekuwa likifanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee kwa miaka mingi na baadaye kuhamia uwanja wa Taifa kwa miaka ya hivi karibuni, kama litafanyika mikoani tu, wao wa Dar es Salaam watakuwa hawajatendewa haki.
“Kama Msama na Kamati yake wataamua tamasha hilo lifanyike mikoani tu, jamani watakuwa hawajatutendea haki kabisa kwa sababu ni tukio ambalo tumelizoea kila mwaka tumekuwa tukienda kupata baraka na watoto wetu,” alisema.
Alisema kama kweli Tamasha hilo halitafanyika jijini Dar es Salaam, litakuwa ni pigo kwa wapendwa ambao mara zote wamekuwa wakiliunga mkono tukio hilo ambalo mbali ya kubeba ujumbe wa neno la Mungu, pia kuyafariji makundi maalum.
Akizungumza  kwa njia ya simu jana kuhusu maoni hayo, Msama alisema ni kweli Tamasha hilo limekuwa likianzia jiji Dar es Salaam kila mwaka kabla ya kwenda mikoani, lakini mwaka huu wamepanga lifanyike mikoani tu kutokana na sababu maalumu.
Alisema, sababu ya kuifanya hivyo ni kutokana na matamasha mengi kufanyika jijini Dar es Salaam, hivyo mpango uliopo ni kuhamia mikoani kwa miaka mitatu mfululizo na kuwataka wadau wa mikoani kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono.

Post a Comment

0 Comments