Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ametoa dola za Marekani milioni 100 (US$ 100m, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 220) kutoka katika Mfuko Mkuu wa Kushughulikia Dharura wa Umoja wa Mataifa (CERF) kwa shughuli za misaada katika maeneo tisa yenye dharura duniani na yasiyo na fedha za kutosha. Tanzania—ambayo kihistoria imepokea mamilioni ya wakimbizi kutoka nchi jirani kwa miaka mingi—imetengewa dola za Marekani milioni 11 (Sawa na shilingi za Tanzania bilioni 24) kutoka katika kiasi hicho kwa lengo la kushughulikia mahitaji ya wakimbizi kutoka Burundi.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akitoa msaada katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo mkoani Kigoma wakati alipofanya ziara mkoani humo
Zaidi ya raia 126,000 wa Burundi wamekimbilia nchini Tanzania tangu mwezi Aprili, 2015, kufuatia machafuko ya kisiasa nchini humo. Huku tayari wakimbizi 64,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wakiwa tayari nchini. Tanzania hivi sasa ina zaidi ya wakimbizi 193,000. Kutokana na ukweli kwamba takribani wakimbizi 1,500 wanawasili nchini kila wiki, inabashiriwa kwamba huenda idadi jumla ya wakimbizi ikafikia 230,000 hadi mwisho wa mwaka 2016. Hali hii inasababisha changamoto nyingi hasa katika kutoa msaada na kinga ya kutosha kwa wakimbizi.
Mchango huu mkubwa kutoka CERF utakuwa muhimu sana katika kutoa misaada ya kiutu kwa wakimbizi wa Burundi wanaoishi katika kambi za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli katika mkoa wa Kigoma, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, na vilevile kwa jamii za wenyeji ambazo zinahitaji kwa haraka huduma bora za maji safi, usafi wa kutosha, matunzo ya afya, chakula na makazi. Sehemu ya fedha hizo pia itatumika kushughulikia mlipuko uliopo wa ugonjwa wa kipindupindu ambao umeathiri mikoa 19 nchini. Fedha za CERF kwa hiyo zitasaidia kuhakikisha kwamba maeneo muhimu zaidi katika dharura yanafanyiwa kazi na kwamba wakimbizi wanapewa kinga na huduma za msingi.
Baadhi ya wakimbizi waliopo katika kambi ya Nyarugusu iliyopo mkoani Kigoma
“Shirika la Kushughulikia Wakimbizi (UNHCR) linakaribisha mchango huu wenye ukarimu mkubwa kutoka CERF ambao unakuja katika kipindi mwafaka kabisa. Utoaji msaada kwa wakimbizi ulikuwa ukikabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha katika mwaka 2015, hali iliyoathiri sana uwezo wetu wa juhudi za pamoja katika mwaka 2015. Tuna imani kwamba hii ni ishara ya kwanza kwa upatikanaji wa fedha nyingi zaidi kwa utoaji msaada katika mwaka 2016. Kwa hakika, mchango huu utasaidia kuziba upungufu mkubwa uliojitokeza katika wito wetu wa sasa na hivyo kushughulikia mahitaji makubwa zaidi ya wakimbizi na jamii za wenyeji,” alisema Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania, Bi. Joyce Mends-Cole.
Kadiri mahitaji ya kiutu yanavyoongezeka, mchango kutoka katika Mfuko Mkuu wa Kushughulikia Dharura wa Umoja wa Mataifa (CERF) umetoa matumaini ya kuendelea kushughulikia dharura ya wakimbizi kutoka Burundi. Tangu mwaka 2006, Nchi 125 Wanachama wa Umoja wa Mataifa na waangalizi, wahisani kutoka sekta binafsi na serikali katika kanda zinazohusika wameendelea kuusaidia Mfuko huo hadi sasa. CERF hadi sasa imetoa jumla ya dola za Marekani bilioni 4.2 (US$ 4.2bn, sawa na shilingi za Tanzania trilioni 9) kwa miradi ya kiutu katika nchi 94. CERF hupokea michango ya hiyari katika mzunguko wa mwaka ili kutoa msaada wa kifedha kwa hatua za kiutu za kuokoa uhai. CERF inapata fedha zake kutoka kwa washirika wengi huku michango mingi zaidi ikitoka: Uingereza, Swideni, Norwei, Uholanzi na Kanada.