Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam leo mchana , kuhusu utendaji wa mahakimu wa mahakama za hakimu mkazi, mahakama za wilaya na mahakama za mwanzo ambapo alitoa siku saba kwa mahakimu 508 watoe maelezo kwani ni wasifunguliwe mashitaka ya nidhamu na kuwajibishwa kwa kufanya kazi chini ya kiwango. Kushoto ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omari Mallungu na kulia ni Jaji Kiongozi wa Tanzania, Shaban Omari Lila. Jaji Chande alitoa kauli hiyo kwenye maonyesho ya wiki ya Sheria yanayoendelea viwanja vya Mnazi Mmoja.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande, akikaribishwa kutembea mabanda mbalimbali kwenye maonesho hayo.
Mkurugenzi Msaidizi Ukaguzi na Maadili Mahakama ya Tanzania, Warsha Ng'humbu (kushoto), akimuelekeza jambo Balbina Mrosso (kulia), kutoka Babati mkoani Manyara aliyetembelea banda la Idara ya Malalamiko kuomba msaada wa kisheria katika maonyesho hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande, akisoma moja ya daftari katika banda la Idara ya Malalamiko kwenye maonyesho hayo. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Malalamiko Mahakama ya Tanzania, Happiness Ndesamburo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande (kulia), akielekezwa jambo katika banda la Divisheni ya Biashara katika maonesho hayo.
Na Dotto Mwaibale
JAJI Mkuu wa Tanzania Othuman Chande ametoa siku saba kwa mahakimu 508 watoe maelezo ni kwanini wasifunguliwe mashtaka ya nidhamu na kuwajibishwa, baada ya kufanya kazi chini ya kiwango.
Jaji Chande ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Mnanzi Mmoja jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Sheria.
Alisema kiwango cha kesi kwa kila Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya ni 250, ambapo Mahakimu Wakazi 121 kwenye mahakama hizo wameamua kesi chini ya 100 mwaka jana.
Alibainisha kuwa kiwango cha kwa kila Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ni 260, ambapo mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo 387 wameamua kesi chini ya 100 mwaka jana.
"Ukiondoa wale ambao wameajiriwa karibuni, wanaofanya kazi kwenye mahakama za mwanzo zisizokua na mashauri mengi au waliyokwenda masomoni kati kati ya mwaka au likizo za ujauzito hawatahusika katika sakata la kujieleza.
"Majaji Wafawidhi nimewaagiza wachambue na kuanisha mahakimu wote walioshindwa kufikia kiwango cha kesi walizopaswa kuamua kesi 250 na kesi 260 kwa mwaka jana na kuwataka watoe maelezo ndani ya siku saba kwa nini wasichukuliwe hatua," alisema Jaji Chande
Jaji Chande alitoa muda wa kukamilika kwa mchakato huo, ambapo walizitaka idara husika ndani ya siku 21 kila kitu kiwe kimekamilika ili ijulikane ni hatua gani wanachukuliwe.
"Mahakama haikubali hakimu ambaye anabembeleza kesi. Hakimu hatakiwi kufanya hivyo anatakiwa asikilize kesi hizo naazimalize. Haiwezekani katika mahakama moja hakimu mmoja anamaliza kesi 800 mwingine anamalizia chini ya 100 hilo halitakubalika kutokana na kasi ambayo tunayo," alisema
Jaji Chande alisema mahakimu hao watapelekwa katika kamati zao kwa hatua ya kujieleza. Kazi kuu ya kamati hizo ni kupeleleza, kuchunguza na kushughulikia mashtaka yote ya nidhamu ya mahakimu.
"Mahakimu wote walioshindwa kufikia malengo ya mwaka la kesi na kushindwa kutoan sababu za kuridhisha kwa nini wameamua idadi ndogo ya kesi kuliko walivyopaswa, ambapo itashughulikiwa haraka na Kamati za Maadili za Mahyakimu kwa mujibu wa sheria na taratibu za haki," alisema
Hata hivyo, Jaji Chande alitoa pongezi kwa mahakimu ambao wamevuka kiwango, ambapo mahakimu 14 wameamua zaidi ya kesi 700 kwa mwaka jana na mahakimu wengine wamesikiliza kesi 915,789 na 778.
Alisema mkakati wao ni kuanza kesi sifuri mwaka unapoanza, kwa sababu kuna baadhi ya mahakama za mwanzo zimekuwa zikimaliza kesi na kuanza mwaka upya.
Jaji Chande alisema Januari 1, 2015 mahakama za mwanzo zilianza na kesi 34,126 na mwaka huu Januari 1 zilianza na kesi 20,431. Kiwango cha kumaliza kesi ukilinganisha na idadi ya kesi zilizosajiliwa 2015 nni zaidi ya asilimia 100. Mahakama ya Mkuranga asilimia 141, Rufiji asilimia 121 na Bukoba Mjini asilimia 224.