Na Mwandishi Wetu
TAMASHA la Pasaka
linalotarajiwa kufanyika mikoa ya Geita na Mwanza mwaka huu limeandaa ujumbe mzito
kuhusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini (Albino).
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti
wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama alisema albino
ni wenzetu hivyo wanapaswa kuthaminiwa na kulindwa kwa mujibu wa katiba
na
sheria za nchini, hivyo Tamasha la Pasaka limebeba ujumbe mzito
utakaotolewa
siku hiyo ya tukio.
“Mikoa ya Kanda ya ziwa mara
kadhaa imegubikwa na matukio ya mauaji ya albino ambayo yanachafua taswira ya
Tanzania ambayo inasifika kuwa kisiwa cha amani na utulivu duniani,” alisema
Msama.
Alisema kuwa mauaji hayo
lazima yakomeshwe kwa kutumia njia mbalimbali lakini kubwa ni kwa njia ya
kuwahamasisha Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa, dini wala kabila
kuhakikisha mauaji ya albino yanakomeshwa.
“Watu wenye ulemavu wa ngozi ni wenzetu hivyo
tunapashwa kuwalinda, kuwapenda na kuwathamini ndiyo maana hata Rais wa tano wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli katika baraza lake la
mawaziri hajabagua kwa kumteua mmoja wa watu wenye ulemavu wa ngozi kuwa
waziri.
Aidha alisema kuwa tamasha
hilo ambalo kauli mbiu yake ni ‘Umoja na Upendo hudumisha Amani ya nchi yetu’ litaanzia
Geita Machi 26, Mwanza Machi 27, Kahama Machi 28 na kuendelea maeneo mengine
nchini.
Msama alisema kuwa maandalizi
ya tamasha hilo yanaendelea vizuri, ikiwa ni pamoja na kupata kibali kutoka
Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) huku
akiwataja waimbaji waliothibitisha kushiriki kuwa ni Bonny Mwaitege na Rose Muhando
ambao wamethibitisha kushiriki Tamasa hilo.
Alimaliza kwa kusema kuwa
waimbaji wa ndani watapewa nafasi kubwa katika tamasha la mwaka huu, huku
waimbaji kutoka nje hawatazidi watatu lengo ikiwa ni kuwapa kipaumbele waimbaji
wa Tanzania.
“Tamasha la Pasaka la mwaka
huu linasukumwa na wadau mbalimbali ambao wanatoa ushauri ikiwa ni lengo la
kuboresha zaidi tamasha hilo,” alisema Msama.
Aidha Msama anasema Tamasha la
Pasaka malengo yake ni kusaidia wenye uhitaji maalum ambao ni pamoja na Yatima,
Walemavu na Wajane kupitia mapato ya milangoni.
“Nawaomba wakazi wa mikoa ya
Geita, Mwanza na Wilaya ya Kahama iliyoko Shinyanga kujitokeza kwa wingi ili
tuwasaidie wenzetu wenye uhitaji maalum,” alisema Msama.
Msama alisema Kamati yake bado
inaendelea na mchakato wa maandalizi ya tamasha hilo ambalo ndio kimbilio la
Watanzania, hivyo tujitokeze kwa wingi ili kufanikisha matakwa hayo.