KITETO YAKABIDHIWA MASHUKA 170


Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Kanali Samuel Nzoka (kulia) akipokea moja kati ya mashuka 170 yaliyotolewa juzi na Meneja wa mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF) wa mkoa wa Manyara, Isaya Shekifu (kushoto) kwenye uzinduzi wa uhamasishaji wa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii CHF.
Na Woinde Shizza,Manyara
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Manyara, umekabidhi mashuka 170 kwenye zahanati ya Kijiji cha Engusero na hospitali ya wilaya ya Kiteto kwa ajili ya kutumiwa kujifunika na wagonjwa wanaofika kulazwa.
Mashuka hayo yalikabidhiwa kwa mkuu wa wilaya hiyo Kanali Samuel Nzoka na meneja wa NHIF wa mkoa huo Isaya Shekifu, kwenye uzinduzi wa uhamasishaji wa kujiunga mfuko wa afya ya jamii (CHF) uliofanyika juzi kijiji cha Engusero.
Akizungumza wakati akipokea mashuka hayo Kanali Nzoka aliushukuru mfuko huo na kuzitaka kaya za eneo hilo kujiunga na CHF ili wajipatie matibabu kwa mwaka mzima kwani kaya moja yenye watu sita italipia sh10,000.

Alisema tatizo la ukosefu wa dawa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitalini litamalizika, endapo kaya nyingi zikijiunga na CHF kwani serikali nayo itaweka mkono wake ili kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa.

Wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo Kanali Nzoka alijitolea sh20,000 kwa ajili ya kuzilipia kaya mbili za watu 12 wa kijiji cha Engusero na Dosidosi na kuungwa mkono na viongozi wanne wa wilaya hiyo waliojitolea sh10,000 kwa kila mmoja.

Kwa upande wake, Shekifu alisema mwanachama wa CHF atanufaika na huduma zote za afya za msingi za kinga na tiba zitolewazo katika zahanati, kituo cha afya na hospitali ikiwemo huduma za wagonjwa wa kutwa na kulazwa.

Alitaja huduma nyingine ambazo zitatolewa kwa mwaka mmoja kwa kuchangia sh10,000 ni vipimo vya maabara, upasuaji kulingana na utaratibu uliowekwa na halmashauri husika na wanachama kupata huduma  bora ya afya.

“Pia watapata huduma ya upasuaji kulingana na utaratibu uliowekwa na Halmashauri zinazoendesha mifuko hii zinapata mapato ya tele kwa tele kutoka serikalini ambayo yatatumika kuboresha huduma za afya,” alisema.

Ofisa uratibu na matokeo wa CHF, Nicholaus Mwangomo alisema mpango huo ulianzishwa kwa sheria namba moja ya mwaka 2001 sura ya 409 ya sheria ya Tanzania toleo la 2002 wa kaya au familia kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua.

Mwangomo alisema sababu za kuanzishwa CHF ni kuiwezesha jamii kumiliki huduma za afya zinazowahusu katika maeneo wanayoishi, kuchangia huduma za afya kwa wananchi na kuboresha huduma za matibabu kwa utaratibu rahisi.


Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post