Mkazi
wa kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga mkoani Tanga, Mohamed Mengwena
akitoa pongezi kwa Serikali kwa kufikisha miundombinu ya umeme kijijini
hapo mbele ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ( hayupo pichani)
katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo
Msimamizi
wa Miradi ya Umeme Vijijini (REA) katika mkoa wa Tanga, Mhandisi Kasim
Rajabu akieleza jambo mbele ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu,
na wakazi wa kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga mkoani Tanga (hawapo
pichani) katika mkutano wa hadhara.
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) pamoja na watendaji kutoka
Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) na serikali wakisikiliza kero mbalimbali zilizokuwa
zinawasilishwa na wanakijiji wa kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga
mkoani Tanga (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara.
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akifafanua jambo mbele ya wanakijiji wa
kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga mkoani Tanga (hawapo pichani) katika
mkutano wa hadhara.
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto mbele) akiendelea na ziara ya
ukaguzi wa miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) katika kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga mkoani Tanga.
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akifafanua jambo kwa wakazi wa kijiji
cha Magumbani kilichopo wilayani Mkinga mkoani Tanga.
Na Greyson Mwase, Tanga
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amezitaka kampuni za Derm Electric,
Njarita, Agwilla na Radi Services kutoa maelezo kupitia Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) ya kutokuendelea na kazi katika maeneo yao ya
miradi wakati walikwishalipwa malipo ya awali na Serikali.
Mgalu
alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki tarehe 16 Desemba, 2017 alipofanya
kikao na watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)- Ofisi ya
Tanga baada ya kubaini wakandarasi hao hawapo katika maeneo hayo ya kazi
na kutohudhuria kikao hicho kama alivyoagiza.
Kikao hicho kilishirikisha pia watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Alisema
kitendo cha wakandarasi kutokuwepo katika maeneo yao ya kazi na
kutohudhuria kikao kama ilivyoagizwa kinakwamisha utekelezaji wa miradi
na hivyo kuutaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kujulisha kampuni
husika kuandika maelezo ya kutokuwepo kwenye maeneo ya kazi na
kukwamisha juhudi za Serikali katika usambazaji wa umeme vijijini.
“
Kama Serikali tumeweka mikakati ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2019- 2021
vijiji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya umeme, sasa inapotokea
baadhi ya wakandarasi wanakwamisha juhudi hizi wakati wamekwishalipwa
na Serikali ni lazima Serikali iwawajibishe kulingana na sheria na
kanuni za nchi,” alisema Mgalu.
Mgalu
aliendelea kuwataka wakandarasi wote nchini kuwepo katika maeneo yao
ya kazi na kukamilisha miradi yao kwa wakati, na kusisitiza kuwa
serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayefanya kazi katika
kiwango cha chini.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri Mgalu aliitaka TANESCO kuwa wabunifu
kwenye ukusanyaji wa madeni na kukamilisha zoezi la uhakiki wa wateja
mara moja ili kukabiliana na changamoto ya upotevu wa mapato ya shirika
hilo.
Alisema
ni jukumu la TANESCO kujiendesha kwa faida kupitia mapato yake na kazi
ya Serikali ni kulipa nguvu shirika hilo kwa miradi mikubwa inayohitaji
fedha nyingi.
Wakati
huo huo, akizungumza katika mikutano tofauti katika kijiji cha
Zangibari kilichopo wilayani Mkinga na katika vijiji vya Mlingano,
Mtindiro, Mpapayu vilivyopo katika wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Naibu
Waziri Mgalu alielekeza wakati wa utekelezaji wa miradi, Wakala wa
Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kuhakikisha taasisi, shule,
nyumba za ibada, hospitali zinapata umeme.
Aidha
alipongeza wananchi wengi katika vijiji vya Zangibari wilayani Mkinga
na Mpapayu wilayani Muheza mkoani Tanga walioonyesha mwitikio mkubwa
wa kuunganisha mfumo wa umeme ( wiring) kwenye nyumba zao na kuwataka
ambao hawajaunganisha mfumo wa umeme kufanya mara moja kwa ajili ya
neema kubwa ya umeme.
Alisema
kwa wale ambao wana nyumba ndogo wanaweza kuwekewa kifaa maalum cha
Umeme Tayari (UMETA) na kuanza kufaidi huduma ya umeme.
Akielezea
mikakati ya serikali katika uboreshaji wa upatikanaji wa umeme wa
uhakika na kwa gharama nafuu, Mgalu alisema kuwa serikali kupitia REA
Awamu ya Tatu inasambaza umeme katika vijiji vyote nchini ambapo
ifikapo mwaka 2019 karibia vijiji vyote vitakuwa na umeme wa uhakika.
Aliendelea
kuelezea mikakati mingine kuwa ni pamoja na matumizi ya nishati
jadidifu kama vile jua hususan katika maeneo yasiyofikiwa na umeme
kutoka Gridi ya Taifa, ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia
maporomoko ya maji ya Mto Rufiji wa Stieglers Gorge na mradi wa
kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi I na Kinyerezi
II.
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia