Friday, August 16, 2024
ANWANI ZA MAKAZI ZAIDI YA 400,000 KUHAKIKIWA MKOANI ARUSHA
Posted by woinde on Friday, August 16, 2024 in HABARI MATUKIO | Comments : 0
Zaidi ya Taarifa za Anwani za Makazi 400,000 zinatarajiwa kuhakikiwa katika Halmashauri Sita za Mkoa wa Arusha katika zoezi la Uhakiki wa Anwani za Makazi lililoanza rasmi Agosti 14 mwaka huu.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 15 Agosti, 2024 na Bw. Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati akizungumzia zoezi hilo linaloendeshwa kwa ushirikiano kati ya Wizara hiyo na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidigitali.
“Mwaka 2022 Serikali iliamua kutekeleza operesheni ya kukusanya taarifa na kutoa Anwani za Makazi iliyojulikana kwa jina la “OPERESHENI ANWANI ZA MAKAZI”. Kupitia Operesheni hiyo, kwa Mkoa wa Arusha tulikusanya taarifa na kutoa jumla ya Anwani za Makazi 442,912 na ndizo zitakazohakikiwa sasa,” amesema Bw. Munaku.
Amesema sambamba na Anwani hizo zitakazohakikiwa, utafanyika usajili wa Anwani za Makazi mapya, matumizi ya anwani husika, na huduma zinazotolewa katika Anwani husika.
Ameitaka jamii kuitikia wito wa Serikali wa kujitokeza kuhakiki na kutoa taarifa zao kwa usahihi kwani kwa kuzingatia malengo mbalimbali ya Maendeleo ya Serikali ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo, Malengo ya Maendeleo Endelevu, Sera na Maelekezo ya Viongozi wa nchi huduma zote zitategemea taarifa za mwananchi kwenye mfumo wa NaPA.
“Unajua kwa sasa ukiambiwa jaza anwani hapa, wengi wanajaza Sanduku la Posta, hiyo siyo sahili kiuhalisia unatakiwa kuandika anwani yako ya makazi kwa kuanza na Namba ya Nyumba, Mtaa, Postikodi (Namba maalum ya Kata) na Wilaya yako, Mfano 55 Mt. Bangulo, 12127 Pugu Station, Ilala ” amesisitiza Bw. Munaku.
Bw. Munaku amesema zoezi la uhakiki wa Anwani za Makazi linakwenda sanjari na kuhamasisha wananchi kuitumia Huduma ya Barua ya Utambuzi Kidigitali itakayomwezesha mwananchi kuepukana na usumbufu mwingi ukiwemo wa kufuata barua hiyo Ofisi ya Serikali ya Mtaa.
Akizungumzia nyumba na majengo yasiyo na vibao vya namba, Mkurugenzi Munaku amesema ni jukumu la mwananchi mwenyewe na kutoa wito kila mmoja aliyepewa namba ya nyumba yake anunue kibao na kukibandika.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia