NCAA YASISITIZA KUENDELEA KUSIMAMIA HAKI ZA WATU KATIKA KULINDA UHIFADHI ENDELEVU.

 


Na Mwandishi wetu.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kusimamia haki za watu katika zoezi la kuhamisha wananchi wanaoishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na  maeneo yote yanayosimamiwa na mamlaka hiyo ili kwenda sambamba na malengo ya milenia ambayo yanahimiza ustawi wa jamii pamoja na  kusimamia uhifadhi ili kukabiliana  na mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza na mwandishi wetu Kaimu Meneja wa Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka hiyo bwana Hamis Dambaya amesema lengo la serikali kuhamisha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora kulingana na malengo ya milenia pamoja na kulinda uhifadhi endelevu.

Amesema kuwa kwa sasa maeneo yote ambayo wananchi wamehama kwa hiyari uoto wa asili umeanza kurejea na hali ya mazingira inaridhisha hivyo ni vyema dunia ikatambua kwamba wananchi wanaoishi ndani ya eneo hilo hawahamishwi ili kupisha shughuli za utalii bali kuimarisha uhifadhi na Maisha ya wananchi kwa kuwezeshwa mazingira bora na salama zaidi nje ya hifadhi.

“Hakuna mantiki yoyote ya hoja ya kuhamisha wananchi kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ikahusishwa na suala zima la utalii, Tanzania ina vivutio vingi vya utalii na sio Ngorongoro pekee, tunachokifanya ni kuhifadhi eneo hilo ambalo kila mtu akifika na kujionea hali halisi ya uharibifu wa mazingira kutokana na ongezeko la shughuli za kibinadamu atakubaliana na nia njema ya Serikali”,amesema bwana Dambaya.

Amesema kwamba idadi ya watu na  mifugo katika eneo hilo imeongezeka kiasi  cha kutisha na ikiwa wananchi hao na mifugo wataendelea kuachwa katika eneo hilo lenye kilomita za mraba 8,292 pekee bila kuelimishwa kuhama kwa hiyari kuna hatari kubwa ya hifadhi hiyo kutoweka na kuathiri mfumo wa  ikolojia kwa maeneo mengine yanayopakana na hifadhi hiyo. 

“Kwa mtu mwenye akili timamu akipiga hesabu ya idadi ya watu 8000 waliokuwepo Ngorongoro mwaka 1959 na mifugo 260,000 hatopinga zoezi hili la kuwaelimisha wananchi zaidi ya 110,000 na mfugo zaidi ya 860,000 katika eneo lenye ukubwa ule ule wa kilomita za mraba 8,292  ili wasihame kwa hiyari”,amesisitiza bwana Dambaya.

 “Wengi wa watu wanaopinga zoezi hilo sio wenyeji wa Ngorongoro, utawakuta wamevaa mavazi ya wenyeji na wengine wakienda katika mataifa mbalimbali kutafuta fedha na kuwarubuni wenyeji wapinge wazo la serikali la kuwahamisha kwa hiyari “,amesisitiza bwana Dambaya.

Dambaya ametoa rai kwa baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa kuacha kuingia mtego wa baadhi ya wanaharakati na badala yake wafike Ngorongoro kujionea ukweli wa mambo na kuona namna zoezi hilo linavyoendeshwa kwa hamasa kubwa bila mwananchi kukamatwa, kushurutishwa wala  kupigwa kama wanavyodai baadhi ya wanaharakati.

Serikali ya Tanzania imeamua kutekeleza zoezi hilo ili kutekeleza maazimio mbalimbali ya kidunia kuhusu utunzanji wa mazingira na kulinda haki za binadamu ambapo katika eneo hilo wananchi wamekuwa wakipoteza maisha kwa kujeruhiwa na kuliwa na wanyama wakali.

Utekelezaji wa zoezi hilo unafuata misingi yote ya sheria, taratibu na kanuni na misingi ya haki za binadamu  na utawala bora.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post