Ticker

6/recent/ticker-posts

Sweden yawataka waandishi wa habari Tanzania kuelimisha umma wakati wa uchaguzi

 

  • Yawataka waandishi kuelimisha umma kuhusu masuala ya uchaguzi.
  • Mafunzo kuhusu akili mnemba (AI), uthibitishaji habari yanukia.

Arusha. Serikali ya Sweden imesema imeridhishwa na utendaji kazi wa wanahabari nchini licha ya changamoto zinazowakibili huku ikiwataka kujitoa kuelimisha umma wakati wa uchaguzi ili kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Balozi wa Sweden nchini Tanzania Charlote Macias ameeleza leo Agosti 6, 2024 kuwa wanahabari ni sehemu muhimu katika kuutaarifu umma kuhusu uchaguzi.

Watanzania wanatarajia kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa mwishoni mwaka huu na uchaguzi mkuu wa 2025 ikiwa ni hatua muhimu za kidemokrasia nchini. 

“Waandishi wa habari wanajukumu kubwa hususan katika uchaguzi unaokuja katika kutoa miongozo na elimu ili wananchi wafahamu jinsi ya kujiandikisha (katika daftari la kudumu la kupiga kura) na aina ya chama cha siasa wachokitaka,” amesema Balozi Macias wakati wa ziara yake katika Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Arusha (APC). 

Licha ya kazi kubwa wanayoifanya waandishi wa habari, balozi huyo ameeleza kuwa bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mafunzo wezeshi yakiwemo yanayohusu akili mnemba (AI) na uthibitishaji habari yanayohitajika zaidi katika kipindi hiki ambacho Taifa linajiandaa na uchaguzi.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, mwanadiplomasia huyo amesema Sweden itaendelea kushirikiana Umoja wa vyombo vya habari Tanzania (UTPC) kuhakikisha waandishi wa habari wanapata mafunzo yanayohitajika. 

Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlote Macias kushoto akizungumza na Kenneth Simbaya, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC na Mwenyekiti wa APC Claud Gwandu alipotembelea ofisi za umoja wa waandishi wa habari mkoani Arusha Agosti 6, 2024. Picha|Lucy Samson/Nukta.

UTPC, Nukta Africa kuwanoa wanahabari

“Tayari tumeanza mazungumzo na wadau kama Nukta Africa ili kuanza mafunzo kwa wanahabari yatakayowawezesha kuripoti habari kwa weledi tutakapoingia kwenye uchaguzi,” amesema Kenneth Simbaya, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC.

Nukta Africa ni miongoni mwa mashirika kinara kwa utoaji wa mafunzo  ya masuala ya kisasa ya uandishi wa habari na mawasiliano yakiwemo yanayohusu takwimu na uthibitishaji habari ili kuongeza umahiri kwa wanahabari na wataalamu wa mawasiliano nchini.

Ndani ya kipindi cha miaka sita, Nukta Africa ambayo ni kampuni ya habari na teknolojia, imeshafundisha waandishi wa habari, wahariri na wadau wa sekta ya mawasiliano zaidi ya 2,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Mtendaji Mkuu wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen ameiambia Nukta Habari kuwa wamejipanga kutoa maarifa na ujuzi muhimu utakaowawezesha wanahabari na wahariri kuwa na uwezo mkubwa wa kuthibitisha habari (Fact-checking) na matumizi ya data na zana za kidijitali kuzalisha habari na makala wakati wa uchaguzi.  

“Tumeshaboresha sehemu kubwa ya mitaala yetu ya mafunzo kwa wanahabari yakihusisha akili mnemba (AI) na kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya habari tunatarajia kuwaongezea uwezo wanahabari wasiopungua 1,000 hadi mwakani,” amesema Dausen. 

Post a Comment

0 Comments