Wednesday, March 2, 2011
MAMBO YALIYOJIRI KATIKA MASHINDANO YA KILIMANJARO MARATHONI
Posted by woinde on Wednesday, March 02, 2011 in | Comments : 0
kiongozi wa twanga akimiliki jukwaa balaaaa
bendi ya Twanga pepeta pia ilikuwepo ikitumbuiza katika mashindano hayo
mmoja wa kiongozi wa kampuni ya soda ya bonite akifurahia naye pia alishiriki mbio hizo
mbio hizi ziliuthuriwa na watu wengi sana wa ndani ya nchi na nje ya nchi
Pia kampuni ya sukari ya TPC walikuwepo na walithamini mashindano wa kushoto ni mmoja wa kiongozi wa kiwanda hicho aliyejulikana kwa jina la Allen Maro yeye alishiriki mbio za kilometa tano
MBIO za Tisa za Kimataifa za Kilimanjaro Marathon zilirindima jana mjini hapa huku ikishuhudiwa Watanzania watatu pekee Banuelia Brighton, Mary Naali na Stephen Huche wakiingia tatu bora mbele ya Wakenya ambao walitawala vilivyo mbio hizo.
Banuelia ambaye ndiye anashikilia rekodi ya Taifa ya Marathoni kamili kwa Wanawake, aliibuka nafasi ya pili katika mbio hizo za Kilomita 42, akitumia saa 3: 02.52 akitanguliwa na mshindi wa kwanza Anna Kamau aliyetumia saa 3:00.16 kutoka Kenya huku nafasi ya tatu ikienda kwa mwenzake Ophra Oruke 3:03.20.
Machungu yaliwazidi Watanzania mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi, pale kwa upande wa wanaume ambako nafasi ya kwanza ilienda kwa Mkenya Kipkemboi Kipsang aliyetumia saa 2: 17.08 akifuatiwa na Julius Kilimo 2:17.10 huku nafasi ikinyakuliwa mwanariadha anayechipukia hapa nchini Steven Huche saa 2:19.24.
Katika Nusu Marathoni wanawake Valentine Kipketer aliibuka kidedea akitumia saa 1:15.08 akifuatiwa na Loren Kitita 1:15.48 wote kutoka Kenya huku Mtanzania Mary Naali akikamata nafasi ya tatu kwa saa 1:15.55.
Kwa wanaume Michael Kemau aliibuka mshindi wa kwanza akitumia saa 1:03.58 akifuatiwa na Leonard Muchare huku nafasi ya tatu ikienda kwa Geofrey Ndungu saa 1:04.04 wote kutoka Kenya.
Washindi katika mbio hizo walizawadiwa zawadi zao na Waziri Nchimbi ambaye mbali ya kuwashukuru waandaaji kwa kumualika pia alitoa shukrani za pekee kwa wadhamini wakuu wa mbio hizi bia ya Kilimanjaro Premium Lager na wadhamini shirikishi kwa mchango wao katika kukuza mchezo wa riadha.
Alisema, jitihada zao za kuwekeza rasilimali na fedha katika mbio hizo zimeleta faida kubwa kwa kuwapa fursa wanariadha wa Tanzania kujipima na wanariadha wa kimataifa na hatimaye kukuza viwango.
“Mwaka kesho mbio hizi zitafikisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake na vilevile kutakuwa na mashindano ya Olimpiki jijini London Uingereza. Nawaomba msituangushe, jitahidi mtuletee medali za dhahabu kwa upande wa marathoni. Mwaka 2006, Samson Ramadhani alipotwaa medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Madola yaliyofanyika Melbourne Australia, sote tulijisikia rah asana na tulifarijika sana. Nawaomba wajitokeze akina Samson wengine watuletee medali za dhahabu,” alisema.
Alisisitiza kuwa, kufanya vema kwa wanamichezo wa hapa nchini Kimataifa kunawapa raha Watanzania, jambo ambalo ni muhimu kwani linawafanya Watanzania kufurahi na kusahau matatizo yao ya kawaida, mbali ya kulitangaza vema jina la nchi kimataifa.
Pia Waziri Nchimbi alielezea kuguswa na maoni ya wadau wakiwamo wa nje ya nchi juu ya utamaduni uliozoeleka kwa viongozi wengi kuthamini soka pekee, hivyo kusisitiza kuwa, yeye si wa aina hiyo ni mdau wa michezo yote na kutoa wito kwa kampuni, taasisi na wadau mbalimbali kujikita katika kuwekeza katika riadha mchezo ambao umeliletea sifa taifa kimataifa kuliko michezo yote.
Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa TBL, Emmy Oriyo alisema, kwa kuwa mwaka kesho mbio hizo zinatimiza mwaka wa 10 tangu kuanzishwa kwake, Kilimanjaro Premium Lager inatoa ahadi kwamba itawekeza zaidi katika mbio hizo ili kuhakikisha maadhimisho ya kumi yanakuja na ongezeko la zawadi na udhamini mkubwa zaidi katika maeneo mengine yote.
“Tunatambua kwamba kukimbia marathoni ni jambo gumu sana na changamoto kubwa, lakini tunafarijika kuona vijana wakiwa kwenye ari na msukumo wa aina yake kuhakikisha wanailetea heshima nchi yetu. Nawapongeza sana wanariadha wote walioweza kushiriki mbio hizi na wale wote walioshiriki kujifurahisha kwa kutuunga mkono, maana uwepo wenu ndio umefanya tukio hili kuwa kubwa kama ambavyo nyote mnajionea,” Alisema Oriyo.
Kwa upande wa burudani bendi ya The African Stars Entertainment ‘Twanga Pepeta’ TMK Wanaume Family na Joseph Payne ‘Mzungu wa BSS’ walipagawisha vilivyo.
Mbio hizo za Kilimanjaro Marathoni zimedhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambao ndio wadhamini wakuu, huku wadhamini shirikishi ni Vodacom Tanzania (5 km Fun Run), DT Dobie, TPC Sugar, Kilimanjaro Water, Tanzanite One, Simba Cement, Keys Hotel, Tanzanite One, Precisionair, KK Security na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), huku waratibu wakiwa ni Wild Frontiers ya Afrika Kusini na Executive Solution ya Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia