Wakazi wa vijiji 10 wilayani Longido mkoani Arusha wanakabiliwa na upungufu wa chakula na janga la umaskini kutokana na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kwa kipindi cha miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2020 mpaka 2023.
Familia nyingi kutoka vijiji vya Orbomba, Oltepes, Ranchi, Orpukeli, Kitumbeine, Kimokowa, Ildonyo, Ngoswaki, Noondoto na Gilailumbwa ndivyo vimeathiriwa zaidi na njaa katika wilaya hiyo yenye jumla ya vijiji 49.
Familia hizi hazina uwezo wa kununua chakula ingawa serikali imepeleka chakula cha bei nafuu ya shilingi elfu 80 kwa gunia la kilo mia moja ila bado hawamudu kununua chakula hicho.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, wilaya ya Longido ina wakazi 175,915 ambapo wanaume ni 82,887 na wanawake 93,028. Asilimia 95 ya wakazi hao ambao ni sawa na watu 167,120 ni wafugaji ambao hutegemea mifugo kama chanzo cha mapato, chakula na mahitaji mengine muhimu kwa maisha ya kila siku.
Kufa kwa mifugo yao kutokana na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kumesababisha upungufu mkubwa wa chakula na kipato kwa kaya hizo.
Mkazi wa kijiji cha Orbomba Sara lesika (51) anasema hali ya chakula kwake ni mbaya sana kwa sababu hana uwezo wa kununua Gunia la mahindi linalouzwa kiasi cha shilingi 80,000/= kwa bei ya serikali kwani alikuwa akitegemea mifugo ambayo kwa sasa hana baada ya kufa kwa ukame.
“Yaani kwa siku tunakula mlo mmoja tu na mara nyingi tunapika uji wa chumvi tunakunywa na kulala kwa sababu bei ya chakula ni ghali sana kwa sasa na hatuwezi kumudu. Debe la mahindi linauzwa shilingi 24,000/= sokoni na ghala la serikali hawauzi kwa debe wanauza kwa gunia kiasi cha 80,000/= tulishazoea kununua sokoni mahindi debe moja kwa shilingi 5000 mpaka 30,000 na gunia 30,000 mpaka 50,000 sasa hapo limepanda Zaidi ya mara mbili ya bei tuliyoizoea,” alisema
Familia hii ni sehemu ya jamii kubwa ya wakazi wa Longido waliokumbwa na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi, na kusababisha ukosefu mkubwa wa chakula kwa kaya hizo na umaskini wa kipato.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia familia zikinywa uji kama chakula cha usiku kwa sababu hautumii unga mwingi ambapo unga kilo moja ukikrogwa uji mzito unaweza kunywewa na familia ya watu 7 mpaka 9.
Afisa Mifugo na Mabadiliko ya Tabianchi Wilaya ya Longido, Nestor Daqarro anasema katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Januari mwaka 2022 hadi Septemba, mifugo 40,000 imekufa kutokana na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Anasema hali ya njaa Longido ni mbaya na ndiyo maana serikali imepeleka chakula hicho cha bei nafuu kuwasaidia wananchi hao. Anabainisha kuwa chakula kilichopokewa wilayani hapo ni tani 736.3, huku akikiri uhitaji ni mkubwa kuliko kiwango kilichopokewa.
Uharibifu wa mazingira wilayani hapo unaonekana kuwa mkubwa, uoto wa asili umepotea kutokana na ukame ulioikumba wilaya hiyo kwa miaka minne mfululizo na kusababisha vyanzo vya maji kukauka.
"Tuna tatizo kubwa la njaa hapa Longido kwani mwaka wa tatu mvua zimenyesha chini ya kiwango na baadhi ya mito ya Koika na Zakiyo imekauka, na kuongeza ukame," amesema.
Serikali imechimba visima na kupeleka maji maeneo ya malisho, ili kuokoa maisha ya mifugo ambayo ndiyo uchumi tegemezi wa kaya za wafugaji hao.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Orbomba, Kashilo Alais anasema serikali ya kijiji imechukua hatua za haraka kudhibiti shughuli za kibinadamu katika nyanda za malisho na kuweka katazo la ukataji wa miti katika kijiji hicho ili kusaidia mvua inyeshe kwa kiwango cha kutosha.
Anasema serikali imechukua hatua hiyo baada ya kuona hali ya ukame na mifugo
kufa na watu kuishi kwa mlo mmoja tu na licha ya serikali kuleta mahindi ya bei nafuu lakini wananchi hao hawamudu kununua mahindi hayo.
“Serikali ya kijiji imelazimika kuomba baadhi ya mashirika yasiyo ya serikali na makanisa yanunue mahindi katika ghala la taifa la chakula na kuwagaia bure wananchi hao,” alisema
Katika Kijiji cha Kimokowa napo hali ya familia kukosa chakula ni kama Orbomba ambapo kumeshuhudiwa ukame mkali lakini pia hata wanyama wa porini wameanza kusogea katika makazi ya watu kusaka maji na kutishia maisha ya wakazi hao.
Leyani Mollel ni mkazi wa Kimokowa, anaiomba serikali kuwasaidia kupewa ruzuku ya mifugo kama Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alivyofanya mwaka 2008 kwa kutoa ruzuku ya mifugo kwa familia baada ya mifugo mingi kufa kwa ukame ili waweze kurejea katika hali nzuri ya maisha.
Diwani wa Kata ya Orbomba, Ndiono Nangeresa Mollel anasema katika kata yake wana mkakati wa kuhakikikisha kunakuwa na matumizi bora ya ardhi kwa kutenga nyanda za malisho na kilimo ili kuinusuru jamii yake na baa la njaa kila mwaka.
“Tumeweka mkakati na utaratibu bora wa matumizi ya ardhi kwa kuwaelimisha wakazi wetu waache tabia ya kuhamahama ili tusiendeleze uharibifu wa maeneo hayo ya malisho,” alisema diwani huyo
Diwani Mollel anaishukuru serikali kuwaletea chakula ambacho wananchi wananunua kwa gharama nafuu kidogo ambapo makanisa na mashirika yasiyo ya kiserikali yananunua na kuwagawaiwa wananchi wao bure na kupunguza kidogo hali ya njaa kwa wakazi hao.
Afisa Miradi shirika la CORDS, Martha Katau amesema wameamua kutoa mahindi ya msaada kwa baaadhi ya kaya wilayani Longido baada ya kubaini kaya nyingi zinakabiliwa na njaa.
“Tunatekeleza miradi kadhaa hapa Longido ukiwemo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, lakini tumebaini kuna upungufu mkubwa wa chakula kwa kaya nyingi na hivyo tumeona tusaidie walau kidogo,” alisema
Anasema wamegawa tani 7.1 za mahindi na maharage tani 3 kwa vijiji viwili vya Ildonyo kaya 165 na Orpukeli kaya 230 ambapo kila kaya ilipatiwa kg 20 za mahindi na maharage kilo mbili ili kusaidia kukabiliana na upungufu wa chakula kwa kaya hizo.
CORDS wanaotekeleza mradi wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda nyasi za asili kwenye nyanda za malisho, kuondoa magugu vamizi na kuvuna maji ya mvua kwa kuweka kinga maji katika maeneo ya malisho wamefanikiwa kupunguza athari za ukame katika maeneo wanaayotekeleza mradi.
Mradi huu wa miaka mitatu ulioanza mwaka 2021 unatarajiwa kukamilika mwaka 2024 unatekelezwa katika vijiji 7 vya Orpukeli, Mundarara, Orgila, Orbomba, Ortepesi Ildonyo na leremata kwa kushirikiana na kamati za mazingira za vijiji husika, umewajengea uwezo wa kukabiliana na ukame pia kupunguza njaa inayowakabili wanavijiji hao.
Mkuu wa mkoa Arusha, John Mongela anasema hali ya ukame imekumba maeneo mengi ya wilaya ya Longido
“Ni kweli tuna tatizo kubwa la ukame wilayani Longido unaotokana na mabadiliko ya tabianchi ambao umesababisha baadhi ya kaya kuwa na upungufu wa chakula,”anasema
Amesema chakula cha bei nafuu kimekwisha pelekwa na serikali wailayani humo ili kuwawezesha wananchi kupata chakula hicho kwa gharama nafuu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt.Seleman Jafo, akiwa katika kikao cha wadau wa mazingira jijini Arusha alisema Serikali imepanga kutumia dola za Marekani million 19.2 ambazo ni sawa na shilingi za kitanzania bilioni 44.16 kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Uamuzi huu wa serikali ukisimamiwa vizuri na miradi kuwafikia kamati za mazingira katika vijiji hivi vilivyoathiriwa na njaa wilayani Longido huenda yakasaidia kudhibiti hali ya uharibifu wa mazingira na ukame iliyotokana na mabadiliko ya Tabianchi.