BREAKING NEWS

Monday, October 17, 2011

KESI YA KUPINGA MATOKEO YA LEMA KUSIKILIZWA JUMATATU

KESI ya kupinga matokeo ya ubunge wa Godbless Lema wa Jimbo la Arusha Mjini,
imeahirishwa hadi Jumatatu ijayo baada ya mahakama hiyo kushindwa
kuwasilisha nyaraka muhimu.



Akiahirisha kesi hiyo jana, Jaji Aloyce Mjulizi, alisema wakili wa
walalamikiwa Method Kimomogoro, aliomba kupewa nakala ya uamuzi mdogo
uliotupilia mbali pingamizi lililowekwa dhidi ya kesi hiyo.



Pia aliomba kupewa nakala ya mwenendo wa shauri hilo lakini hadi kesi hiyo
inatajwa jana asubuhi upande wa walalamikiwa haukuwa umepata nakala hizo.



“Nathibitisha drafti na nakala ya mwenendo wa shauri la pingamizi ipo kwenye
faili nilikabidhiwa leo,” alisema Jaji Mjulizi.



Katika uamuzi wake wa kuahirisha kesi, Jaji Mjulizi alimwagiza msajili wa
mahakama kutoa nakala hizo kwa wadaiwa na wadai kabla ya kuanza kusilikiza
kesi hiyo wiki ijayo.



Pia alimwagiza msajili wa wilaya kutoa taarifa ya shauri hilo kwa mujibu wa
sheria na kubandika kwenye ubao wa matangazo mahakamani hapo na kuomba
ukumbi mkubwa wa kusikilizia kesi hiyo kutokana na idadi kubwa ya watu
wanaopenda kwenda kusikiliza.



Maagizo mengine aliyotoa ni kumtaka msajili kuweka utaratibu wa mwenendo wa
shauri hilo kusikilizwa kwa vipaza sauti ili kuruhusu watu wengine
watakaoshindwa kuingia ndani ya ukumbi waweze kusikiliza.



Jaji Mjulizi alitoa amri hizo baada ya wakili wa wadai Alute Mughwai,
kuikumbushia mahakama hiyo kuhusu muda uliopangwa kusikiliza kesi hiyo hadi
Desemba kuwa ni mdogo.



Kutokana na hali hiyo aliomba mahakama hiyo iandae utaratibu wa kuomba muda
wa nyongeza, kutoa taarifa ya siku ya kesi kwenye ubao wa matangazo, na kesi
hiyo isikilizwe kwenye ukumbi mkubwa zaidi.



“Hiki chumba hakifai kwa usikilizaji wa kesi hii, tumejazana na hewa
haitoshi, inatakiwa ipande toka chini hadi kichwani,” alisema na kuongeza,
“tunahitaji uwanja mpana wa kufanya kazi yetu.”

Pia Wakili Mughwai alilalamikia suala la usalama mahakamani hapo lakini
wakati akitoa ombi hilo, sauti za kumsonya zilisikika kutoka kwa watu
waliokuwa wamekaa nyuma yake.



“Mheshimiwa Jaji, unasikia jinsi ninavyosonywa, hii inaonyesha wanataka
nisiseme na huu sio utaratibu wa kuendesha kesi mahakamani,” alisema.



Hata hivyo, Jaji Mjulizi alisema, “hawakusonyi wewe ila wanaisonya
mahakama,” na baada ya kusema hivyo watu hao walisikika wakipiga makofi,
lakini baadaye Jaji alionya kwamba anayesonya anaidharau mahakama.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates