BREAKING NEWS

Saturday, October 22, 2011

NDEGE NDOGO YAANGUKA ARUSHA

NDEGE ndogo ikiwa na marubani wawili imeanguka ambapo mmoja ,Ally
Harun (24) alifariki na mwingine Liliani Koima amejeruhiwa vibaya na
kulazwa hospitali ya rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro Moshi.

Ndege hiyo yenye namba za usajili 5 H/QTE mali ya kampuni ya World
Quality travel & Tours ya jijini Arusha ilianguka wakati ikielekea
kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada
ya kushindwa kutua kwenye uwanja mdogo wa ndege wa Arusha kutokana na
kukosekana taa kwenye njia ya kutua na kuruka uwanjani hapo .

Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa hapa , Akili Mpwapwa jana
alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo kwenye kijiji cha Samaria
wilayani Arumeru siku ya alhamisi majira ya Saa 1:55 usiku alipokuwa
akisubiri ruhusa ya kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Kilimanjaro, KIA.


Alisema kuwa rubani Kolina anaendelea kupatiwa matibabu kwenye kwenye
hospitali ya KCMC ambako hali yake inadaiwa kuendelea kuimarika
ambapo mwili wa haruna umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti
cha hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru .


Akielezea tukio hilo Mpwapwa alisema kuwa ndege hiyo ilikuwa
imetokea jijini Dar Es Salaam ambapo ilifika katika uwanja mdogo wa
Arusha lakini akashindwa kutokana na uwanja huo kukosa huduma ya taa
kwa sababu ambazo hazijajulikana hadi sasa iwapo ni mgawo wa umeme au
hitilafu ya kiufundi.



Alisema kuwa marubani hao walielekezwa kwenda kutua KIA ambapo
walifanya mawasiliano na waongoza ndege wa uwanja huo na kuwaruhusu
baadaye walipoteza mawasiliano na ndipo ikapatikana taarifa za ajali
hiyo .

Mpwapwa alisema kuwa ndege hiyo ilianguka jirani na nyumba ya Maria
Akyoo ambapo mbuzi wake watatu walikufa na banda lake lililokuwa
pembeni ya nyumba hiyo kuharibiwa kabisa .

Taarifa zilizopatikana kwa walioshuhudia ajali hiyo zinaeleza kuwa
kabla ya kuanguka, ndege hiyo ilionekana ikizungukazunguka kwa muda
mrefu maeneo ya karibu na kijiji hicho katika kile kinachodaiwa
kusubiri maelekezo ya kuruhusiwa kutua.

Sababu za kukosekana kwa taa uwanjani hapo zilishindikana baada kila
mfanyakazi aliyeulizwa kutokuwa tayari kutoa ushirikiano kwa waandishi
wa habari huku wakikataa kusema alipo meneja wa uwanja.
Hata baada ya kupatikana kwa njia ya simu yake ya kiganjani, meneja wa
uwanja huo, Simon Kimiti alikataa kuzungumzia ajali hiyo na kuelekeza
atafutwe mwenzake wa KIA aliyedai ndiye mhusika.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates