AFP YAMKINGIA KIFUA RC MGHWIRA


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama cha Wakulima Tanzania (AFP) kimeponda vikali maamuzi ya kumvua uongozi aliyekuwa Mwenyeliti wake wa Taifa wa  ACT Wazalendo  Anna Mghwira kwasababu ya kuteuliwa kwake na Rais Dk John Magufuli kuwa mkuu wa Mkoa Kilimanjaro na kusema uamuzi huo umeongozwa na chuki na si wa kistaarabu. 


Pia AFP kimesema haikustahili kwa ACT 'Wazalendo kupitisha uamuzi huo hasa iiizingatiwa  hata kiongozi mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe alipokuwa Chadema aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya  mikataba ya madini na Rais Jakaya Kikwete lakini hakuvuliwa uongozi wala uanachama.

Msimamo huo umeelezwa jana na  Mwenyekiti wa Taifa wa AFP Said Soud Said kufuatia uamuzi wa kamati kuu ya ACT - Wazalendo kutangaza kumvua wadhifa wake Mghwira na kumteua mwanachama mwingine kukaimu nafasi yake . 

Soud alisema kitendo  kilichofanywa na Rais Dk Magufuli ni cha kistaarabu ambacho kinaanza kufungua milango na kulifanya Taifa na wananchi wazoee  na kutoshangaa kuona viongozi toka upinzsni wakifanya kazi pamoja na chama tawala  bila misuguano. 

Alisema hata mwaka 1964 mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume kwa kujali maslahi mapana na kujenga umoja wa kitaifa, aliunda Serikali iliowashirikisha baadhi ya wapinzani wa ASP.

"Cha ajabu nini hadi ACT wamvue wadhifa Mwenyekiti wao, chama hicho kimepata hadhi baada ya wanachama wake wawili kuteuliwa na Rais na kutumikia serikali, hakuna hoja zenye mashiko katika sakata hili ila ni chuki na jazba zenye ghera "Alisema Soud. 

Mwenyekiti huyo wa AFP alisema Mzee Karume alimshirikisha Abdulrahman Mohamed Babu, Ali Abdallah Ameir, Ali Sultan Issa na Kanali Ali Mahfoudh huku akimteua Dk Salim Ahmed Salim kuwa Balozi nchini Misiri  akiwa kijana mdogo wa miaka 21 .

Aidha kiongozi huyo alisema hata Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa Makamo wa Kwanza wa Rais zanzibar mwaka 2010 /2015 huku akiwa Katibu Mkuu wa CUF hali kadhalika hivi sasa viongozi wa ADC, AFP na TADEA wameshirikishwa katika serikali ya Umoja wa kitaifa inayoongozwa na Rais wa Zanzibar  Dk Ali Mohamed Shein.

"Babu aliposhiriiishwa baadae akateuliwa  kuwa Waziri katika Serikali ya kwanza ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  , Kanali Mahfoud akapelekwa jeshini, lengo la Mzee Karume na Mwalimu Julius Nyerere ni kulishushwa  joto la mifarakano na hasama "Alisema.

Pia Soud alimsifu Rais Dk Magufuli na kusema midhali Serikali yake inakusudia kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, bado ana haki, fursa na uamuzi wa kumteua mwanachama wa chama chochote ambaye ni makini na muadilifu amsaidie kazi. 

"ACT kimsingi kimeshirikishwa katika serikali ya Jamhuri ya Muungano,ikiwa ina wanachama mmoja ni Katibu Mkuu wa Wizara ya serikali na mwingine Mkuu wa Mkoa, hiyo ni hadhi inayowapa jeuri ya kujivunia,  huo ni mwanzo mzuri uliohitaji kuheshimiwa "Alisema Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo alipotajiwa  madai ya ACT ni kwamba Rais Dk Magufuli kabla ya uteuzi huo hakuwashiriiisha wala  kufanya majadiliano nao, Soud alisema hadhi ya Rais haina ukomo wala mipaka hivyo anaweza kumteua au kumvua wadhifa mtu yeyote atakayeona hakubailani  naye serikalini .

"Haijafikia mahali CCM na serikali yake hasa Bara kujadiliana na vyama vya upinzaji namna ya uundaji wa serikali,upinzani bado haujapevuka na kupata uwakilishi, ukiteuliwa na chama chako kuingizwa serikalini jua mmebahatika"Alisisitiza Soud 


About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.