Ticker

6/recent/ticker-posts

WAKAZI WA MANISPAA YA UBUNGO WAMPONGEZA JPM KWA MAAMUZI MAGUMU KWA MANUFAA YA WATANZANIA


Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli

Wakazi wa Mitaa tofauti tofauti katika Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam ukiwemo Mtaa wa kimara, Ubungo, Sinza, Mabibo, Mwembechai na Magomeni wamempongeza Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli kwa kuunga mkono maoni/Mapendekezo ya Ripoti ya pili ya wachumi na wanasheria iliyofanya uchunguzi wa madini yaliyo kwenye makontena zaidi 250 yenye mchanga wa dhahabu yaliyokuwa yamehifadhiwa katika bandari kavu ya MOFED (zamani ZAMCARGO) iliyopo Kurasini jijini Dar es salaam.

Rais Magufuli ameunga mkono ripoti hiyo kutokana na ukiukwaji wa sheria za nchi na upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali kupitia biashara ya Makinikia na madini yanayosafirishwa nje ya nchi.

Wananchi hao wamesifu uwepo wa Rais Magufuli huku wakieleza kuwa Tanzania imefanikiwa kupata kiongozi imara na madhubuti atakayeweza kuifanya Tanzania kuwa ya neema na mafanuikio makubwa.

Mapendekezo hayo ya kamati maalumu yaliyoungwa mkono na Rais Magufuli ni ishirini na moja kama ifuatavyo

1. Serikali, kupitia Msajili wa Makampuni ichukue hatua za kisheria dhidi ya kampuni ya Acacia Mining Plc ambayo imekuwa inaendesha shughuli zake nchini kinyume na matakwa ya Sheria.
2. Serikali idai kodi na mrahaba kutoka kwa makampuni yote ya madini ambayo yamekwepa kulipa kodi na mrahaba stahiki kwa mujibu wa sheria.

3. Serikali iendelee kuzuia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi mpaka hapo makampuni ya madini yanayodaiwa yatakapolipa kodi, mrahaba na tozo stahiki kwa mujibu wa sheria.
4. Serikali ianzishe utaratibu utakowezesha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia (smelter) ili kuondoa upotevu wa mapato na kutengeneza ajira kwa watanzania.

5. Serikali ifanye uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliokuwa Mawaziri, Wanasheria Wakuu wa Serikali na Manaibu wao, Wakurugenzi wa idara za mikataba, na Makamishna wa madini, wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini na watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa makampuni ya madini, makampuni yaliyohusika kuandaa nyaraka za usafirishaji wa makinikia(Freight Forwarders(T)Ltd na makampuni ya upimaji wa madini kwa kuvunja sheria za nchina upotoshaji.

6. Serikali ifute utaratibu wa kupokea malipo ya mrahaba ya asilimia 90 na kusubiri malipo ya asilimia 10 kulipwa baadaye wakati makampuni hayo ya madini huyauza madini hayo na kupewa fedha taslimu kwa mkupuo.

7. Serikali ifanye uchunguzi kuhusu mwenendo wa Watumishi wa idara ya walipakodi wakubwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kushughulikia madai ya kodi ambayo Mabaraza ya Rufaani ya Kodi na Mahakama zimekwisha yatolea uamuzi na vilevile ichunguze mienendo ya watumishi wa mabaraza ya Kodi kwa kutotolea maamuzi ya kesi za kodi kwa muda mrefu kuhusu mashauri yaliyochukua muda mrefu kukamilika katika vyombo hivyo.

8. Benki Kuu ya Tanzania ifuatilie malipo ya fedha za kigeni yanayotokana na mrahaba kwa mauzo ya madini.

9. Serikali ianzishe utaratibu wa kulinda maeneo ya migodi na viwanja ndege vilivyopo vigodini ili kudhibiti vitendo vya hujuma vinavyoweza kuwa vinafanywa na makampuni ya migodi ikiwemo utoroshaji wa madini.

10. Sheria iongeze kiwango cha adhabu zilizoainishwa kwa makosa ya ukiukwaji wa Sheria ya Madini na Sheria za Kodi.

11. Serikali kupitia wataalum wabobezi katika majadiliano na mikataba (expert in negotiation and contract) wapitie mikataba yote mikubwa ya uchimbaji madini ipitiwe (review) na kufanya majadiliano na makampuni ya madini ili kuondoa misamaha yote ya kodi isiyokuwa na tija kwa taifa na badala yake kuweka masharti yenye tija kwa pande zote mbili kwa kuzingatia maslahi ya nchi;

12. Sheria iweke kiwango maalum cha asilimia ya hisa ambazo zitamilikiwa na Serikali katika makampuni yote ya madini nchini. Aidha, Sheria ielekeze Serikali kufanya majadilaino ili kuwezesha Serikali kununua hisa katika makampuni ya uchimbaji madini ili kuiwezesha kupata mapato zaidi na ushiriki katika maamuzi muhimu katika biashara ya madini.

13. Serikali iunde chombo cha kusimamia biashara ya usafirishajibidhaa nje ya nchi kupitia bandari kama ilivyokuwa kama lilivyokuwa shirika la NASACO ili kudhibiti biashara haramu na kuondoa mianya ya ukwepaji kodi.

14. Sheria itamke bayana kuwa madini ni mali asili ya watanzania na iwekwe chini ya udhamini na uangalizi wa Rais kwa manufaa ya watanzania.

15. Sheria itamke bayana kuwa mikataba yoyote ya uchimbaji mkubwa wa madini (Mining Development Agreement) isiwe ya siri na lazima yaridhiwe na Bunge kabla ya kuanza kutekelezwa.

16. Sheria itoe masharti ya wazi ya kuzingatiwana iondoe uhuru wa mamlaka ya (discretionary powers) za Waziri wa Nishati na Madini, kamishna wa madini na maafisa madini wakanda katika utoaji wa leseni za uchimbaji madini.

17. Sheria ya madini iweka masharti kwamba mwombaji wa leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini lazima yaoneshe mchanganuo wa kina kuhusu namna mafunzo kwawazawa yatakavyotolewa kwa lengo la ajiri kama wataalam na kuchukua nafasi za uendeshaji wa migodi husika na kupunguza au kuondoa kabisa wataalam kutoka nje ya nchi.

18. Sheria ielekeze makampuni ya madini kuweka fedha zinazotokana na mauzo ya madini katika benki zilizopo nchini ili kuimarisha uchumi wa nchi na kuondoa mianya ya ukwepaji wa kodi na tozo mbalimbali.

19. Serikali ipitie na kufanya marekebisho au kufuta na kubadili kabisa Sheria ya Madini na Sheria za Kodi ili kuondoapamoja mambo mengine masharti yote yasikuwa na manufaa kwa taifa ikiwa ni pamoja na masharti yaliyomo kwenye kifungu thabiti (stability provision).

20. Serikali igharimie nakutoa mafunzo kwa watumishi wa Serikali ili kuwapatia uelewa na weledi katika nyanja ya majadiliano na uendeshaji wa mashauri yatokanayo na mikataba ikiwemo ya mikataba ya madini (skills in negotiation and arbitration).

21. Serikali kupitia Kamishna wa Madini iwe inafanya ukaguzi wa mara kwa mara kaw makampuni ya madini ili kujihakikishia uzingatia au ukiukwaji wa Sheria na taratibu za uendeshaji na kuchukua hatua ipasavyo.

IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO
HALMASHAURI YA MANISPAA YA UBUNGO

Post a Comment

0 Comments