MKUU wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro amempongeza Mwenyekiti
Mtendaji wa Taasisi ya Goodall Foundation ya Uingereza, Andrew Goodall
kwa kuamua kutumia fedha zake kuboresha elimu hapa nchini.
Goodall ametumia fedha zake kuinua elimu katika wilaya za Ngorongoro
na Arusha na hivyo kumtaka mfanyabiashara huyo tajiri wa tatu nchini
Uingereza kusambaa zaidi katika wilaya nyingine nchini.
Aidha, amewataka walimu wakuu wa shule zote za msingi za serikali
mkoani hapa kuwa waunganishi kati yao na serikali katika kutatua kero za
walimu na kuboresha elimu kwa faida ya Watanzania wote.
Daqarro alisema hayo jana kabla ya kukabidhi vyeti vya walimu wakuu
25 wa shule za msingi za serikali waliohudhuria kozi ya mafunzo ya
uongozi ya miezi sita iliyoandaliwa na Taasisi ya The Robbin &
Sylvia Goodall Foundation inayoongozwa na tajiri huyo wa Uingereza.
Daqarro alisema serikali inamhakikishia ushirikiano mkubwa katika
kuboresha elimu nchini ili kuendesha mafunzo ya kozi ya uongozi,
kuzifanyia ukarabati shule za msingi na kujenga maabara za kisasa kwa
ajili ya wanafunzi Naye Goodall aliyeambatana na mama yake mzazi Sylvia,
alisema uamuzi wa kuwekeza katika elimu nchini ni mapenzi yake na
wafanyakazi wa taasisi hiyo kwa Watanzania.
Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi sana na inatakiwa kuwa nchi ya
kwanza Afrika kwa kuwa na uchumi mkubwa na imara hivyo ameamua kutumia
kozi hiyo kuelimisha walimu na wanafunzi kufahamu umuhimu wa rasilimali
za nchi na kuzitunza.
Alisema elimu bora ndio msingi mkubwa katika kutunza rasilimali,
hivyo basi taasisi yake imejikita kuboresha elimu ili watu wafahamu
umuhimu wa rasilimali na kuzitunza. Goodall alisema alisikitishwa pale
alipoona wanafunzi wanasoma kwa kukaa chini, chakula cha shida shuleni,
umbali mrefu kutoka shule hadi nyumbani na ndio maana ameamua kutoa
msaada wa madawati na kuzifanyia ukarabati shule zilizokuwa katika hali
mbaya.
Mwaka huu, taasisi yake imepanga kutumia Sh biloni tatu kwa kazi
hiyo.
Awali, mkuu wa wilaya alisema kero zilizoko mashuleni zinapaswa
kutatuliwa na pande zote mbili za walimu wakuu kwa kushirikiana na
serikali ili wanafunzi wapate elimu bora na kuiachia serikali pekee ni
kuionea.
Aliwataka walimu wakuu kutumia kozi hiyo kubadilika na kufanya kazi
kwa weledi na kuacha kuwa na urasimu usiokuwa na tija. Daqarro alisema
hakuna mwalimu mkuu aliyechaguliwa kufundisha kijiji na mwingine
kufundisha mjini tu hilo halitawezekana na aliwataka walimu wakuu
kubadilika kwa hilo na kuwataka kufanya kazi eneo lolote liwe la kijiji
au mjini.
Naye Ofisa Elimu Taaluma na Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Ngorongoro,
Anyamisye Mahali alisema mafunzo hayo yanaweza kubadilisha ufundishaji
katika shule za msingi na wanafunzi kuwa na uelewa mpana kwa faida yao
ya baadaye.