Na Umar Mukhtar , Zanzibar
Chama
cha ADA Tadea kimewataka Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
kuvihamu vyombo hivyo vinaendeshwa kwa taratibu zake maalum kwa kufuata
kanuni zilizotungwa kisheria hivyo Mbunge au Mwakilishi atakayekiuka
taratibu zilizopo lazima ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni.
Pia
Chama hicho kimesema kila mhimili wa dola una taratibu na kanuni zake
kwani bila uwepo wa kanuni za uendeshaji, vyombo hivyo vingekabiliwa
na mabishano, misuguano pia mivutano isio ya suluhisho wala ukomo.
Hayo
yameelezwa jana mjini unguja na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na
Mawasiliano kwa Umma wa ADA Tadea, Rashid Yussuf Mchenga kufuatia uamuzi
wa Spika wa Bunge Job Ndugai kuwasimamisha wabunge wawili wa Chadema,
Halima Mdee na Ester Bulaya.
Mchenga
alieleza kuwa Mabunge na Mabaraza yote ya Wawakilishi duniani huongozwa
na kanuni zilizotungwa na kujipangia baada ya kupitishwa katika
taratibu halali na kwamba Mbunge au Mwakilishi atakayekiuka huadhibiwa
bila kutazamwa usoni .
"Ingelikuwa
Mahakama ni bustani basi maji yake ni ushahidi kwa mujibu wa sheria,
tufahamu kuwa utawala huongozwa kwa kufuata sheria na katiba huku
mabunge yote duniani yako chini ya kanuni zake zilizotungwa na
kukubaliwa "Alisema Mchenga.
Aidha
alisema ni makosa kusema Mbunge au Mwakilishi fulani amefukuzwa kwa
utashi wa Spika kwasababu Spika hutoa maamuzi kwa mujibu wa kanuni
zilivyo na kwenye kamati ya Nidhamu na Maadili kiongozi wa upinzani huwa
ni mjumbe mshiriki.
"Spika
ni kiti si mtu, hana maamuzi wala uwezo wa kutenda na kuamua jambo
ikiwa suala hilo halina nguvu za kikanuni, Mbunge au Mwakilishi
anapotimuliwa na kupewa adhabu ni wazi atakuwa amevunja na kukiuka
kanuni halali "Alisisitiza.
Kiongozi
huyo wa upinzani aliwataka Wabunge na Wawakilishi kujiheshimu kwasababu
hadhi na daraja zao mbele ya jamii hazilingani na makuli wa
bandarini,wateja wa unga au wapiga debe kwenye vituo vya mabasi ya
daladala.
Mchenga
alisisitiza kuwa kila mhimili una taratibu zake, mfumo wake na kanuni
husika hivyo kutofuata na kutii taratibu hizo ni kuiitafutia matatizo ya
kujitakia na yamapomkuta madhila mbunge au Mwakilishi hastahili kupewa
pole au kusikitikiwa.
"Haiwezekani
vyombo vya Bunge au Baraza la Wawakilishi vikaendeshwa kama kundi la
walevi wako katika vilabu vya pombe, vyombo hivyo vina staha na miiko
yake, jamii inawakilishwa na vyombo hivyo na katu si busara uhuni na
ukorofi kuwa sehemu ya bunge au baraza "Alisisitiza .
Akitoa
mfano alisema Bunge maalum la katiba lilipoundwa na kukosekana mfumo
wa kanuni lilikuwa kama soko kuu la kariakoo au la darajani zanzibar kwa
kuhanikiza kelele, mipasuko na malumbano lakini kanuni pale
zilipotungwa kila mmoja aliheshimu na kutii taratibu.
"Tulizoea
kuwaona wabunge wa nchi moja jirani wakirushiana viti na kupigana ngumi
mara kadhaa, tokea waboreshe kanuni zao sasa wamekuwa waungwana,
wastaarabu na wenye kutambua hadhi na heshima yao ndani ya bunge
"Alieleza Mchenga .
Hata
hivyo Mkurugenzi huyo wa ADA Tadea aliiwahimiza na kuwashauri wabunge na
wajumbe wa Baraza la Wawakiiishi kufuata na kuheshimu kanuni
zilizotingwa na kwamba vituko, mikasa na mizozo wanayoianzisha kimsingi
haitoi taswira njema katika jamii kulingana na daraja zao.