WATU 20 wamekamatwa kwa kukutwa na shehena ya bangi gunia 168 katika
kitongoji cha Engendeko, Kijiji cha Losinoni wilayani Arumeru mkoani
hapa.
Akithibitisha kukamatwa kwa shehena hiyo ya bangi alfajiri ya kuamkia
jana, Kamishna wa Intelijensia wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na
Dawa za Kulevya nchini, Fredrick Kibute alisema ofisi yake ilishirikiana
na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutoka Oljoro ili kufanikisha
kazi hiyo.
“Tulipata taarifa kutoka kwa raia wema na wiki iliyopita tukatuma
kikosi maalumu kwa ajili ya uchunguzi na baada ya kupata taarifa za
uwepo wa bangi hiyo tulipanga safu ya kikosi kazi kwa ajili ya kuja
Arusha kukamata bangi hiyo ambayo awali wananchi hao waligomea uongozi
wa wilaya baada ya kutakiwa kukisalimisha,” alisema Kibute.
Kwa mujibu wa Kibute, aliondoka saa nane usiku jana kuelekea katika
kijiji hicho akiwa na kikosi maalumu kutoka ofisini kwake, wanajeshi
pamoja na polisi na majira ya saa 10.00 alfajiri waliwasili katika
kitongoji hicho na kuanza msako wa nyumba kwa nyumba.
“Kijiji cha Losinoni hasa kitongoji cha Engendeko ni eneo la kipekee
ambalo limetia fora katika kilimo cha bangi na kuificha bila kukamatwa,
lakini tulitumia intelijensia ya hali ya juu kuhakikisha tuwakamata wote
pamoja na bangi walizokuwa nazo ndani ya nyumba zao za kuishi,”
alifafanua.
Kamishina Kibute alitumia fursa hiyo kuwaonya wananchi wa Wilaya ya
Arumeru kuacha mara moja tabia hiyo ya kulima bangi na kuwataka wasome
alama za nyakati badala ya kufanya kilimo hicho kwa mazoea.
“Wanaojihusisha na kilimo cha bangi waache wasome alama za nyakati,
ukiwa bondia usiogope ngumi za usoni ngumi zetu ni Sheria Namba Tano ya
Mwaka 2010 ambayo sasa inasimamiwa kikamilifu ili kuhakikisha
tunadhibiti dawa za kulevya hapa nchini kwani imeharibu maisha ya vijana
wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa,” aliongeza.
Kwa upande wake, Luteni Moses Gimonge kutoka Kikosi cha 833 Oljoro,
alisema kazi hiyo haikuwa rahisi kutokana na kijiji hicho kuwa na milima
na mabonde makubwa ambapo wananchi walitoka ndani ya nyumba zao na
kukimbia, lakini waliwakabili kikamilifu na kuhakikisha wanatia mbaroni
bila ya hata mmoja kukimbia.
Serikali ya Wilaya ya Arumeru tangu Agosti mwaka jana ilianza
kupambana na kudhibiti kilimo cha bangi katika kata 14 na vijiji 22
ambavyo vilikuwa vinategemea kilimo cha bangi kama kitega uchumi cha
kujipatia kipato. Alisema baadhi ya vijiji vimeachana na biashara hiyo
haramu na kuanza kulima mazao aina ya mahindi, alizeti na pareto