Chuo
Cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kwa mara ya kwanza kimeanzisha
Masomo ya Shahada ya kwanza (Degree) katika fani za Uhazili na Utunzaji
wa Kumbukumbu, Taarifa na Nyaraka.
Kufuatia
kuanzishwa kwa masomo ya Shahada ya kwanza katika Chuo cha Utumishi wa
Umma Tanzania, Mkuu wa Chuo Dkt. Henry Mambo ametoa wito kwa watumishi
wa umma na Watanzania wenye sifa kuchangamkia nafasi hizo za masomo kwa
manufaa yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Dkt.
Mambo alisema masomo hayo ya Shahada ya kwanza yataanza Mwezi
Septemba,2017 katika Matawi ya Dar es Salaam na Tabora, nayo ni hatua
kubwa kwa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania katika kuwaendeleza
Watumishi na Watanzania Kitaaluma.
Kwa
upande wa sifa za kujiunga na masomo hayo ya shahada ya kwanza, Dkt.
Mambo alisema muombaji anatakiwa kuwa na elimu ya kidato cha sita pamoja
na ufaulu katika masomo mawili au Diploma katika fani husika yenye
ufaulu au GPA alama 3.
Mkuu
wa Chuo pia aliendelea kufafanua kwamba Masomo hayo ya ngazi ya Shahada
yameanzishwa ili kuhakikisha kwamba watumishi wa umma na Watanzania
wenye sifa za kujiunga wanakabiliana na changamoto zinazojitokeza katika
soko la ajira kufuatia mabadiliko ya teknolojia na mifumo mbalimbali ya
utendaji kazi.“Kutokana na mabadiliko hayo ni vema Watumishi wa Umma na
Watanzania wenye sifa kwa ujumla nao wakapata mafunzo ambayo
yatawawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali katika soko la
ajira,”.
Kuhusu
shahada ya Uhazili na Utawala, Mkuu wa Chuo alisisitiza kwamba Wahitimu
wataweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za mawasiliano katika
utendaji wao wa kazi wa kila siku na hivyo kuwawezesha kufanya kazi kwa
ufasaha katika sekta ya umma na hata sekta binafsi. “Mafunzo hayo pia
yatawawezesha wahitimu kumudu nafasi ya Maofisa Wasaidizi Waandamizi
ambao watafanya kazi katika taasisi mbalimbali hapa nchini na hata nje
ya nchi kulingana na soko la ajira litakavyowahitaji” alisema.
Kuhusu
Shahada ya Utunzaji Kukumbukumbu, Taarifa na Nyaraka, Mkuu wa Chuo cha
Utumishi alibainisha kwamba mafunzo hayo yatawawezesha wahitimu
kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha mkubwa zaidi katika eneo hilo na
hivyo kuchangia katika uendelezaji na ukuaji wa Taaluma ya Utunzaji
Kukumbukumbu, Taarifa na Nyaraka.
Mafunzo
ya ngazi ya shahada (Degree) yatatolewa kwa muda wa miaka mitatu,
wakati yale ya Diploma na Cheti yataendelea kutolewa kwa kipindi cha
miaka miwili na mwaka mmoja kama kawaida na akatoa wito kwa watumishi wa
umma na watu wote wenye sifa za kujiunga na masomo hayo kuchangamkia
fursa hizo kwa kujaza fomu za kujiunga na Chuo zinazopatikana katika
matawi yote ya Chuo cha Utumishi wa Umma ya Dar es Salaam, Tabora,
Singida,Mtwara, Tanga na Mbeya, na katika tovuti ya Chuo www.tpsc.go.tz
Katika
kongamano la Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama Cha Makatibu Mahsusi
Tanzania (TAPSEA) lililofanyika hivi karibuni Mkoani Dododma, Makamu wa
Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa kufungua Mkutano huo, aliwataka
makatibu Mahsusi hao kuichangamkia kozi hiyo, kwa kuwa ni fursa nzuri
kwa Makatibu Mahsusi na itawasaidia sana katika kuongeza weledi na
ufanisi kazini.
Nae
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mh. Angellah Jasmine Kairuki, ambae pia alihudhuria Kongamano hilo
na ambaye Chuo cha utumishi wa Umma kiko chini ya Wizara yake, aliwatoa
hofu waombaji wa kozi hizo mpya zilizoanzishwa na Chuo cha Utumishi wa
Umma Tanzania kwa kusema Ofisi yake inalitambua hilo na inalifanyia kazi
suala hilo ili Wahitimu watakapomaliza mafunzo yao ya miaka mitatu(3),
waweze kutambulika nafasi zao katika Muundo wa Utumishi wa Umma. Hivyo
akawahimiza Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu Taarifa na Nyaraka
kuchangamkia nafasi hizo.
Mwandishi
wa gazeti hili pia aliweza kuongea na Katibu Mkuu wa TAPSEA, Festo
Melikiory ambaye alisema kuwa kuanzishwa kwa kozi hizo ni fursa kwa
Watanzania hususan Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu na kwamba ni
matumaini yake kuwa kozi hizo zitaongeza weledi na ujuzi miongoni mwa
watumishi wa umma na watanzania kwa jumla. “Hiki kilikuwa ni kilio chetu
cha siku nyingi, sasa kimesikilizwa, ni matumaini yangu kuwa Makatibu
Mahsusi wengi wataichangamkia fursa hii,”alisema.
Katibu
Mkuu huyo wa TAPSEA alitoa wito kwa Makatibu Mahsusi kuichangamkia kozi
hiyo kwani itaongeza uwezo wao wa utendaji wa kazi.Alisema kozi hiyo ni
fursa nzuri kwa Makatibu hao kwani itawasaidia sana katika kuongeza
weledi na ufanisi kazini.
Baadhi
ya Watumishi wa Umma na wananchi wamekipongeza Chuo cha Utumishi wa
Umma kwa kuanzisha masomo ya Shahada katika fani hizo na kusema kwamba
mafunzo hayo ni hatua kubwa katika mchakato wa kuendeleza taaluma ya
elimu hapa nchini.
Pamoja
na kutoa Mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi majukumu mengine ya Chuo
cha Utumishi wa Umma Tanzania ni kutoa Huduma ya Shauri za Kitaaluma,
Tafiti na Machapisho mbalimbali yanayohusiana na uendeshaji wa Utumishi
wa Umma.
Mafunzo
ya muda mfupi yanatolewa kwa Watumishi wa Umma pamoja na watumishi wa
sekta binafsi ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao ya
kila siku kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Mafunzo
yatolewayo na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yamejikita katika
maeneo ya Menejimenti, Utawala na Uongozi, Usimamizi wa Rasilimali Watu,
Utunzaji wa kumbukumbu Taarifa na Nyaraka, Usimamizi wa Fedha,
Uendeshaji wa Ofisi, Ununuzi na Ugavi, Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano .