Muuguzi Mkuu mkoani Mwanza Agness Hassan, akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani 2017, kimkoa Mwanza yakifanyika uwanja wa Nyamagana hii leo Mei 28,2017.
#BMGHabari
Wanafunzi wa
kike kutoka shule mbalimbali Jijini Mwanza wameiomba serikali kusaidia ujenzi
wa viwanda vya pedi za kisasa vitakavyosaidia pedi hizo kuuzwa kwa beo nafuu.
Hayo
yamesemwa kwenye risala yao iliyosomwa na mwanafunzi Edna Ignas kutoka shule ya
msingi Malulu, kwenye maadhimisho ya Siku ya hedhi duniani yaliyofanyika jana katika
uwanja wa mpira Nyamagana.
Aidha
wameomba ujenzi wa viwanda hivyo vya pedi uendani na kupunguza ama kuondoa
kabisa kodi kwenye mauzo ya kodi hizo, hatua ambayo itasaidia kuuzwa kwa bei
nafuu na hivyo kuwafikia wasichana wote hususani wanaotoka kwenye kaya zenye
uwezo mdogo wa kiuchumi.
Mkurugenzi
wa Shirika la Tanzania Youth With New Hope in Life Organization (TAYONEHO) la
Jijini Mwanza, Dkt.Iman Tinda, amesema suala la hedhi limekuwa na changamoto
kubwa ikiwemo baadhi ya mabinti wanafunzi kukosa masomo wakati wa hedhi.
Amesema
mabinti hupoteza vipindi darasani kati ya siku mbili hadi saba kwa mwezi, siku
86 kwa mwaka na hivyo kuwa kikwazo kwao kimasomo ambapo ni vyema wadau wa elimu
wakaungana pamoja ili kuvunja ukimya juu ya suala la hedhi na hivyo kuwasaidia
mabinti kuondokana na changamoto wanazokumbana nazo katika kipindi hicho.
Naye Mratibu
wa Shirika la Plan International mkoani Mwanza, Emmanuel Asaph, amebainisha kwamba
elimu ya hedhi tayari imewafikia wanafunzi 250 kutoka shule 10 za msingi Jijini
Mwanza pamoja na waalimu wa kike na kiume 20 ambao wamefunzwa namna bora ya
kuwa msaada wa kwanza kwa mabinti watakaokumbana na changamoto za hedhi wawapo
shuleni.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Muuguzi Mkuu mkoani Mwanza Agness Hassan,
amesema halmashauri zote mkoani Mwanza kwa kushiriakana na kamati za shule
zinafanya juhudi za kuhakikisha mazingira yanakuwa salama ikiwemo upatikanaji
wa maji safi ili kuwasaidia mabinti kujiweka nadhifu pindi wawapo kwenye hedhi.
Maadhimisho
hayo mkoani Mwanza yameratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali la TAYONEHO la
Jijini Mwanza kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la Plan International
pamoja na lile la SVC Mwanza.
Lengo ni uvunja
ukimya juu ya masuala ya hedhi ikiwemo kuondokana na dhana potofu kwamba hedhi
ni ugonjwa pamoja na namna bora ya kuhakikisha mtoto wa kike anajiweka katika
hali ya usafi ili abaki shuleni badala ya kukosa masoko kila apatapo hedhi.
Siku ya
hedhi duniani ilianza kuadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014 baada ya
kuidhinishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa ambapo ni mara ya kwanza
kuadhimishwa mwaka huu 2017 nchini Tanzania ikiwa na kauli mbiu isemayo
"Elimu juu ya hedhi hubadili kila kitu".
Mkurugenzi wa Shirika la TAYONEHO, Dkt.Iman Tinda, akizungumza kwenye maadhimisho hayo
Mwanafunzi Edna Ignas kutoka shule ya Msingi Malulu Jijini Mwanza, akisoma Risala kwa niaba ya wnafunzi wenzake kwenye maadhimisho hayo
Wanafunzi wakiwa kwenye maadhimisho hayo
Tazama Video hapo chini