Ticker

6/recent/ticker-posts

TANGA CEMENT YATOA MIFUKO ELFU MOJA YA SARUJI UJENZI NYUMBA ZA POLISI

 
Meneja Biashara wa Kampuni ya Tanga Cement Bw. Peet Brits akikabidhi mifuko ya Saruji Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo



Ujenzi wa nyumba za polisi jijini hapa unaendelea
Na Woinde Shizza, Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa, limepokea jumla ya tani hamsini sawa na mifuko elfu moja ya Saruji yenye thamani ya shilingi Milioni kumi na Mbili na Laki Tano toka kampuni ya Saruji yaTanga (Tanga Cement) ili ziweze kusaidia ujenzi wa nyumba za Askari wa Jeshi hilo ambalo hivi karibuni walipatwa na majanga ya moto yaliyosababisha nyumba za familia 13 kuungua na kuteketeza karibu kila kitu.
Akipokea shehena hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo aliishukuru Kampuni ya Tanga Cement kwa kujitoa na kutambua mchango wa askari katika kuimarisha usalama, na kuahidi kusimamia ili ujenzi huo kasi yake iongezeke.
Alisema mbali na Kampuni hiyo pia aliwaomba watu wengine binafsi pamoja na Makapuni mengine waige mfano toka kwa kampuni hiyo kuisaidia jamii hasa katika sekta mbalimbali kama vile elimu, afya na majanga kama haya.
Kamanda Mkumbo pia alitumia fursa hiyo kushukuru watu binafsi , makampuni, taasisi pamoja na majeshi ya Ulinzi na Usalama kama vile Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi Kilimanjaro, Chuo cha Polisi Moshi na Jeshi la Magereza.
Wengine ni kiwanda cha Magodoro cha Tanfoam, kiwanda cha A to Z, Ofisi ya Mwanasheria mkoani hapa, Green Valley School na Kampuni ya Otterlo Business Corporation Ltd (OBC) pamoja na watu binafsi ambao walitoa msaada wa fedha, Chakula, Saruji nguo pamoja na Magodoro.
Kwa upande wake Meneja Biashara wa kampuni hiyo Bw. Peet Brits alisema kwamba, wao kama kampuni wameweka mkazo kusaidia katika elimu, afya, maendeleo ya Jamii pamoja na mazingira lakini kwenye majanga mbalimbali kama vile ajali za moto.
Alisema kwamba anafahamu kazi zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika kudumisha usalama ambapo unasaidia kuvutia mazingira mazuri ya kibiashara hapa nchini. Alisema wametoa msaada huo ili usaidie kujenga makazi ya familia za askari.
Bw. Brits alisema anajua walichochangia hakiwezi kutosheleza lakini wanaamini kitasaidia kwenye ujenzi wa nyumba hizo na kuzitaka kampuni pamoja na taasisi kusaidia Jeshi la Polisi ambalo linaimarisha usalama hali ambayo inasaidia kuweka mazingira mazuri ya kibiashara.
Familia 13 za Jeshi hilo mkoani hapa zilikosa makazi siku ya tarehe 27/09/2017 baada ya nyumba zao zilizopo katika moja ya Kambi za Polisi kuungua kwa moto uliotokana na hitilafu ya umeme ulitokea muda wa saa 12:45 Jioni.

Post a Comment

0 Comments