BREAKING NEWS

Friday, October 6, 2017

DC MTATURU AKUTANA NA WATAALAMU WA KILIMO IKUNGI KUJADILI UBORESHAJI SEKTA YA KILIMO.


Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu amekutana na kufanya kikao cha kazi na wataalamu wa Kilimo, Mifugo, Ardhi, Maliasili na mazingira kubaini kwa pamoja mbinu bora za kuwasaidia wakulima kuzalisha mazao ya chakula na biashara kwa wingi.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Maafisa kilimo na Mifugo, Maafisa Ardhi, Maliasili na Mazingira, Maafisa Ugavi wa Kata sambamba na Maafisa Tarafa, Mtaturu amesema kuwa bado uzalishaji wa mazao ni mdogo katika Wilaya ya Ikungi ukilinganisha na hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kuwa na ardhi nzuri.

Amewataka wataalamu hao wa kilimo kuwasaidia wakulima ili kuiwezesha Sekta ya Kilimo, kutoka kilimo cha kujikimu kuwa kilimo cha kibiashara, kitakachowezesha kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kupunguza umasikini kwa watanzania Sambamba na kujitosheleza kwa chakula.

Mtaturu amesema ili kilimo kiwe kizuri na chenye tija kwa wananchi, Wataalamu wanapaswa kuzingatia uwepo wa pembejeo na mbegu bora za kisasa na kuhuisha kilimo cha umwagiliaji kwa kuandaa mpango wa kujenga skimu za umwagiliaji.

Ameongeza kuwa serikali imetoa tani 20 za mbegu za kamba katika Wilaya ya Ikungi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo ambapo zitagawanywa kwa wakulima ili msimu wa kilimo unapoanza tayari kusiwe na kucheleweshwa kwa mbegu hizo.
Pia amewaagiza maafisa ugani kuwa na mashamba darasa kwani kupitia wao yatawasaidia wakulima kuwa na uelewa mkubwa katika kuongeza ufanisi wa kilimo chenye tija.

Aidha, amesema Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imeanzisha huduma zake kanda ya Kati Dodoma ambapo mikopo ya aina mbalimbali hutolewa kuwezesha wakulima kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.

Mtaturu amesema ni vyema kama wataalamu wa kilimo watatumia nafasi hiyo kuwaunganisha wakulima na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa Masoko na kuongeza Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo.

Katika kikao hicho cha kuwakumbusha majukumu wataalamu hao Mtaturu amewataka kuandaa mpango kazi wa mazao ya kilimo hususani mazao ya chakula na biashara.

Mtaturu amewaelekeza wataalamu hao wa kilimo kuwasisitiza wananchi katika maeneo yao kuanza kulima mazao ya kipaumbele yaliyoelekezwa na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa ambayo ni zao la Pamba, Korosho, Chai, Kahawa na Tumbaku.

Amesema pomoja na mazao hayo ya kipaumbele lakini pia wananchi wanapaswa kuendelea kuongeza nguvu katika mazao yanayostawi kwa wingi Wilayani humo ikiwa ni pamoja na zao la alizeti, mtama, mahindi na zao la dengu.

Katika upande mwingine Mtaturu ameshauri wataalamu wa Mifugo kutilia msisitizo Ufugaji wa kisasa (Ziro Grazing) kwa kutembelea na kupata utaalamu wa Ufugaji na mbegu Bora za ya Ng'ombe wa kisasa kwa wataalamu katika Rachi ya Taifa ya Kongwa (NARCO) na LITI iliyopo Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Sambamba na hayo pia Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza heka 1500 ambazo ni kichaka kuandaliwa utaratibu kwa ajili ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa kilimo.

Naye Afisa Kilimo na Mifugo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ndg Ayoub Sengo amepongeza kasi ya uwajibikaji ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu kwa ufanisi wake kusaidia kuonyesha njia jambo ambalo linapelekea kubadili fikra za wakulima na wananchi kwa ujumla.

Sengo amempongeza Mkuu huyo wa Wilaya ya Ikungi kwa kuwezesha kupatikana muwekezaji ambaye atakayepewa heka 1000 na serikali ya kijiji kwa ajili ya kilimo cha korosho zao ambalo litakuwa na tija kwa pande zote mbili kwani pia wananchi watanufaika na huduma za ugani.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates