BREAKING NEWS

Sunday, April 17, 2011

MWANRY AWAWEKA CHINI YA ULINIZI WACHAFUZI WA MAZINGIRA



Naibu waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanry akiwa amesimamia kuwekwa chini ya ulinzi vijana watatu aliowakata ,ambao majina yao hayakuweza kufahamika mara moja,kwa kosa la kula magembe kwenye gari na kutupa maganda barabarani,kushoto ni mkuu wa polisi wilaya ya Arusha Zuberi Mwombeji



NAIBU waziri wa Tawala za mikoa na serikali za mitaa(TAMISEMI), Agrey Mwanri ameuagiza uongozi wa halmashauri ya jiji la Arusha ,kuhakikisha kwamba ,jiji hilo linakuwa safi muda wote ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wale wote wanaojihusisha na utupaji ovyo wa taka ngumu.



Mwanri alienda mbali zaidi kwa kuwataka viongozi hao kuandika barua za kujiudhulu, mara moja, iwapo shughuli ya kutunza mazingira katika mji wa Arusha , zimewashinda.



Aliyasema hayo mjini hapa, baada ya kuwakamata na kuwaweka chini ya ulinzi vijana watatu aliowashuhudia wakila maembe ndani ya gari aina ya Fusso na kutupa maganda ovyo katika barabara ya uhuru mjini hapa.



Alisema kwamba inatia aibu kwa jiji la Arusha ambalo linavitega uchumi vingi na linaingiza wageni wa kila aina wakiwemo mashuhuri , kuona linatoa harufu mbaya za taka na taka ngumu zikizagaa ovyo barabarani bila kuchukua hatua yoyote.



‘’ivi nyinyi viongozi mnafanya nini ,kama hamuwezi kazi ya kuung’arisha mji andikeni barua mjivue gamba, wenzetu wa Moshi kwa nini wamewashinda ,nendeni kwa mkurugenzi wa Moshi , Mama Kinabo, mkajifunze usafi,alisema na kuongeza



‘’Haitapendeza kuona mgeni akitembea huku akiwa ameziba mdomo na kitambaa kutokana na harufu mbaya ya uchafu ,hii hatuwezi kuivumilia hata kidogo ,mwambieni na mkurugenzi wetu,nitatuma wasaidizi wangu waje wafuatilie hatua mlizozichukua’’alisema Mwanri alipokuwa akiwaeleza baadhi ya viongozi wa manispaa hiyo waliofika eneo la tukio.



Aidha aliwataka viongozi hao wa manispaa kutumia askari wao kukamata mtu yoyote atakayeonekana kutupa taka ovyo na kuwatoza faini za papo kwa papo,hali ambayo alisema itakomesha uchafu ndani ya jiji hilo .



Mwanri aliamuru vijana hao akiwemo dereva na gari hilo, kuwekwa ndani katika kituo cha polisi na kufunguliwa mashtaka .Hata hivyo alimwagiza mkuu wa polisi wa wilaya (OCD) Zuberi Mwombeji kuhakikisha kuwa ,vijana hao hawaachiwi bila kulipa faini kwa mujibu wa sheria za manispaa hiyo na kuonya kwamba iwapo wataachiwa kiujanja ujanja ,taarifa zifikishwe kwake ili achukue hatua zaidi za kinidhamu dhidi ya wahusika.



Hata hivyo baadhi ya wananchi walimweleza wazi, naibu waziri huyo kwamba ,uchafu uliokidhiri katika jiji la Arusha unatokana na uzembe wa viongozi wa manispaa hiyo kwa kushindwa kusimamia kikamilifu uzoaji wa taka ngumu zinazolundikana maeneo mbali kwa muda mrefu na kujikuta zikioza na kutoa harufu kali.



‘’mheshimiwa waziri uchafu huu unasababishwa na viongozi wa manispaa ,kwanza gari lao la taka huwa linamwaga uchafu ovyo barabarani,halafu wao wenyewe ni wachafu hawazoi uchafu uliopo kwenye masoko ukiingia sokoni unaweza kutapika’’alisema mwananchi mmoja kwa niaba ya wenzake.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates