Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro amesema kuwa
ataelekeza fedha zote za rambirambi kwa wafiwa badala ya kuzipeleka kwa
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Aidha amehoji ni kwanini fedha za rambirambi zilizochangwa
kwaajili ya msiba wa wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja
kuchotwa Sh.milioni 1.5 kupelekwa kama rambirambi katika msiba wa bwana
na bibi harusi waliosombwa na maji Kata ya Sambasha iliyopo Wilayani
Arumeru kama pole.
Meya, Lazaro aliyasema hayo Jijini Arusha wakati
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya
kuachiliwa na Jeshi la Polisi leo majira ya saa 12:30 asubuhi kisha
kwenda ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya
Kaskazini.
Amesema fedha hizo za rambirambi zitakazochangwa na watu
mbalimbali kisha kuletwa kwake kama Meya wa Jiji la Arusha, atazielekeza
kwa wafiwa moja kwa moja badala ya kwa RC Gambo kwani RC huyo
anaonekana kutumia fedha hizo kwa malengo mengine na kumtuhumu kuwa
anachukua fedha zinazochangwa na kupeleka kwenye misiba ambayo ilitokea
kipindi cha nyuma kama rambirambi.
Amesema wafiwa wanahoji ni kwanini fedha zilizobaki
zilazimishwe kujenga jengo la Wagonjwa Mahututi (ICU) Sh,milioni 56
huku akijua kabisa fedha hizo zimechangwa kwaajili ya rambirambi kwa
wafiwa.
“Yani hili jambo ni la ajabu sana nimefika shuleni kutoa
rambirambi na si mimi bali nimewasindikiza umoja wa shule binafsi na
nikaomba viongozi wa dini wafanye sala kwaajili ya kuanza kutoa fedha
hizo lakini cha ajabu nakamatwa kwa kosa gani ,na mimi nasema
sitaelekeza fedha kwa RC Gambo ambazo ni za rambirambi bali zikija
kupitia ofisi yangu nitazielekeza kwa wafiwa ambao wapo kwenye kila
Kata,”alisema na kuongeza;
"Mimi ni Diwani wa Sokoni One, Wazazi waliofiwa wako 6
kwenye kata yangu, Diwani wa Olasiti ana familia 11 zilizofiwa… na
Diwani mwingine Credo ana familia 6 zilizopoteza watoto, kwahiyo
nikawaambia Madiwani wangu wahakikishe hizo familia zinakuwepo pale
shuleni.
"Moja ya vitu Wadau hao walitaka kuwe na maombi na
nilimuandaa Padri wa Kanisa Katoliki, Mchungaji wa KKKT na kiongozi wa
BAKWATA kutoka Olasiti, kabla ya zoezi la kukabidhi rambirambi mkononi
kwa Wafiwa Polisi walivamia.
"Maswali tulikua tunahojiwa ni kwanini fedha hizi
hatujazipitisha kwa mkuu wa mkoa? nataka Watanzania wajue kwamba hakuna
Kiongozi wa Serikali aliyefariki, walifiwa Wananchi wa kata zetu… mimi
Meya wa jiji nimefiwa na Wananchi wangu"
Naye Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema tukio lile ni tukio la aibu
na wakati Fulani walimshauri RC Gambo awe mtu mzima akiendelea na mambo
haya hatafika mbali.
Awali Mei 19, 2017, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho
Gambo wakati akipokea msaada uliochangwa na wananchi kupitia tovuti ya
wezesha sasa ambapo alipokea msaada wa takriban shilingi milioni 4
alisisitiza kuwa wanasiasa waache kutumia msiba kwa kuingiza siasa kwani
hakuna fedha yoyote ile iliyoliwa na pia wapo katika harakati za
kuwatumia fedha wazazi pamoja na timu ya wataalam wa afya walioongozana
na watoto wa Lucky Vicent ambao ni majeruhi wanaotibiwa nchini Marekani
kama fedha za kujikimu na kiasi kilichobaki hadi sasa ni zaidi ya Sh,
milioni 56 ambazo kunakamati ndogo ya wazazi iliyoteuliwa ambao wataamua
zitumikaje kwaajili ya kumbukumbu za watoto hao.