UTAMADUNI KAHAMA WAWAITA WAKAZI WAKE TAMASHA LA PASAKA


Na Mwandishi Wetu
OFISA Utamaduni wa Mji wa Kahama Julius Kambarage amewaomba wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kujitokeza kwa wingi kwenye Tamasha la Pasaka mjini Kahama litakalofanyika Machi 28 kwa sababu mji huo haujawahi kukutanisha makundi  ya walemavu mbalimbali kama wa viungo na ngozi.
Kambarage anasema Tamasha la Pasaka ni nafasi kubwa kwa wenye uhitaji maalum ili waweze kujimudu kimaisha ambako kampuni ya Msama Promotions inatekeleza kazi ya Mungu ipasavyo.
“Kampuni ya Msama Promotions inatekeleza juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli ambaye anatekeleza majukumu yake kwa kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’, alisema Kambarage.
Kambarage anawasisitizia kampuni ya Msama Promotions, Tamasha hilo mwaka huu usiwe mwisho, liendelee na miaka ijayo kwa sababu ujio wao ndio uponaji katika maisha yao.
“Tamasha la Pasaka ni sehemu ya maandalizi ya maisha mapya kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya ziwa ambayo yataongeza mapenzi zaidi baada ya kutawaliwa na mauaji ya albino na walemavu,” alisema Kambarage.
Tamasha la Pasaka linatarajia kuanza Machi 26 mkoani Geita, Machi 27 Mwanza na Machi 28 Kahama.
Viingilio katika tamasha hilo ni shilingi 5000 kwa wakubwa na shilingi 2000 kwa watoto.
           

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post