MWENYEKITI wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex
Msama amekoshwa na Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuwa mgeni rasmi kwenye
Tamasha la Pasaka litakalofanyika Mwanza Machi 27 na kueleza kwamba ni faraja
kwao.
Akizungumza na
waandishi wa habari juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo,
Alex Msama alisema Nape ni mmoja wa walezi wa tamasha hilo ambalo mwaka huu
linatarajia kuanzia Geita Machi 26 na kumalizikia Kahama Machi 28.
“Maandalizi
kuelekea Tamasha la Pasaka yanaendelea vema na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa
waziri Nape, hivyo wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wajiandae kupokea ujumbe wa
neno la Mungu kupitia viongozi wa dini na waimbaji wa muziki wa Injili,”
alisema Msama na kuongeza.
“Tunafurahishwa
na Waziri Nape kukubali kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Pasaka, kwa sababu
ni mmoja wa wanaoweza kusaidia mipangilio ya Matamasha yanayoandaliwa na
Kampuni ya Msama Promotions kama ilivyokuwa Tamasha la Krismasi lililofanyika
mwaka jana,” alisema Msama.
Aidha Msama
anatumia fursa hiyo kuwaweka bayana waimbaji waliothibitisha kushiriki Tamasha la Pasaka ambao ni pamoja na Rose
Muhando, Bonny Mwaitege, Upendo Nkone, Jesca BM Honore, Christopher Mwahangila,
Joshua Mlelwa, Sifael Mwabuka, Jenipher Mgendi, Kwaya ya AIC Makongoro ya
Mwanza na Kwaya ya Wakorintho wa pili kutoka Njombe.
Anavitaja viingilio
katika tamasha hilo litakalofanyika mikoa ya Kanda ya Ziwa ni Sh. 5,000 kwa
wakubwa na kwa watoto Sh 2,000. Msama alisema maandalizi ya tamasha hilo
yanaendelea vema na kutoa wito kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kujitokeza
kwa wingi.