· Pampu yadaiwa kupelekwa Morogoro, yeye asema iko kijijini
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya
Chato, Bw. Peter Ngunura kwa kosa la kumdanganya mbele za watu na kumpa
taarifa za uongo juu ya pampu ya maji iliyodaiwa kupelekwa Morogoro.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Machi 16, 2016) alipokuwa
akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Chato waliojitokeza kumsikiliza
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wilayani
Chato, mkoani Geita.
Waziri
Mkuu ambaye amewasili mkoani Geita kwa ziara ya siku mbili akitokea
mkoani Kagera, alisimamishwa na wakazi wa kijiji cha Kalebezo, kata ya
Nyamirembe, wilayani Chato na kukuta mabango yaliyokuwa yakidai maji
safi na kuelezea uharibifu wa pampu ya maji.
Katika
maelezo yao, wakazi hao walimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi wa maji
kwenye kata hiyo ulishakamilika lakini pampu yao imechukuliwa na
kupelekwa Morogoro jambo lililosababisha wakose maji kwa muda mrefu.
Kwa
sababu alikuwa hajafika Chato mjini na hakuwa na taarifa sahihi za
mradi huo wa maji, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao kwamba analibeba
jambo hilo na atafuatilia hadi aelezwe ni kwa nini pampu hiyo imepelekwa
Morogoro. Akiwa kwenye mkutano wa hadhara, ndipo suala la maji
likaibuka tena na Waziri Mkuu kuamua kuchukua hatua hiyo.
“It’s
unethical (ni kinyume cha maadili) kumdanganya kiongozi wako.
Nimekuuliza mara mbili mbili kama una uhakika kuwa pampu hiyo ipo
ukasema una uhakika kuwa ipo. Nimemtuma diwani na vijana wangu wakacheki
wakasema hakuna pampu,” alisema Waziri Mkuu na kumwita Diwani huyo
jukwaani ili atoe majibu.
“Pale
kulikuwa na pampu mbili; moja ni ya kuvuta maji kutoka kwenye kina
kirefu na kuyapeleka kwenye pump house na nyingine ni ya kuvuta maji
kutoka kwenye pump house na kuyapeleka kwenye tenki kubwa la kuhifadhia
maji. Ile ya kutoa maji kwenye kina kirefu ndiyo haipo, wataalamu
wanajua wameipeleka wapi,” alisema Bw. Charles Manoni ambaye ni diwani
wa kata ya Nyamirembe ambayo kijiji cha Kalebezo kimo.
Waziri
Mkuu alisema ahadi ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuwatumikia wananchi
kwa uadilifu. “Lazima watumishi wa umma wabadilike na kuanza
kuwatumikia wananchi kwa dhati. Hatuwezi kuwa na watumishi waongo ambao
wanamdanganya hata Waziri Mkuu.”
“Kuanzia
sasa, Engineer atakaa pembeni, polisi na TAKUKURU wamchunguze. Asitoke
Chato hadi uchunguzi ukamilike. Nataka kujua nani alichukua hiyo pampu
na kwa kibali gani. Tukijiridhisha atarudi lakini kwa sasa hivi akae
kando,” alisema.
Mapema
jana mchana, akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Geita na
wilaya ya Chato mara baada ya kupokea taarifa zao kwenye ukumbi wa
Halmashauri, Waziri Mkuu alimpa fursa Mhandisi huyo aeleze nini
kimetokea kuhusu pampu inayodaiwa kupelekwa Morogoro lakini akakanusha
na kudai kuwa ipo palepale kijijini.
“Una
uhakika na hayo unayoyasema? Hiyo pampu ipo kweli kijijini? Nikienda
nitaiona?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa mara mbili na mhandisi huyo
kwamba ana uhakika asilimia 100 kwamba pampu ipo na wala haijaenda
Morogoro.
Alipotaka
kujua ni kwa wananchi wa kijiji kile hawana maji kutokana na ubovu wa
pampu hiyo, alijibiwa kwamba mradi ule ulikuwa chini ya mamlaka ya maji
ya mji wa Bukoba (MBUWASA) ambako wilaya hiyo ilikuwepo zamani kabla ya
kuhamishiwa kwenye mkoa mpya wa Geita mwaka 2012.
Mhandishi
huyo alisema amekuwa akifuatilia fedha za matengenezo kutoka kwa
Mkurugenzi wa MBUWASA bila mafanikio, ndipo Waziri Mkuu akamuagiza aende
nje ya ukumbi huo akapige simu na kumletea majibu ni lini fedha hizo
zitapatikana ili wananchi wa kijiji kile waendelee kupata maji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, MACHI 17, 2016.