Staa Diamond Platnumz
Staa wa muziki nchini Naseeb Abdul Juma a.k.a Diamond Platnumz ametakiwa kutoka Jijini Dar es salaam na kurejea Mkoani Kigoma alikozaliwa, ili kuwasaidia Wasanii chipukizi katika Mkoa huo.
Mbali na Diamond, Staa mwingine alietajwa ili atoke Jijini Dar es salaam na Kurejea Mkoani kwake ni Farid Kubanda a.k.a Fid Q, ambae ametakiwa kurejea Jijini Mwanza ili kusaidia kuukuza muziki wa Mwanza.
Mbali hao mastaa hao ambao wametajwa live majina yao, pia mastaa wote waliohamishia shughuli zao za sanaa Jijini Dar es salaam wametakiwa kurejea katika Mikoa yao ili kuondoa mrundikano wa wasanii katika Jiji hilo.
Hayo yalisemwa juzi ijumaa Jijini Mwanza na Msanii Chipukizi Joseph Stanford a.k.a Rich4D, katika hafla ya kumpongeza kwa ushujaa wake wa kutembea kwa miguu kutoka Jijini Mwanza hadi Jijini Dar es salaam, kwa ajili ya Kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kutambua mchango wa wasanii nchini na kuwajumuisha katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
"Wasanii wakubwa watoke Jijini Dar na warudi Mikoani kwao ili wawasaidie wasanii chipukizi wa Mikoani. Diamond arudi Kigoma. Fid Q arudi Mwanza. Hii itaondoa mrundikano wa wasanii wakubwa Dar na hivyo kupeleka fursa za sanaa mikoani". Alisema Rich4D.
Matembezi ya Miguu ya Msanii Rich4D yalianza Januari 16,2016 yakihusisha mikoa minane sawa na Kilomita 1,200 na yalifikia tamati Februari 10,2016, lakini adhma yake ya kuonana na rais haikuweza kutimia baada ya rais kuwa katika majukumu mengine ya kitaifa ambapo aliekuwa Katibu Mkuu Ombeni Sefue aliahidi msanii huyo kuonana na rais.
Wadau mbalimbali waliosaidia kufanikisha matembezi hayo akiwemo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana Raphael Shilatu pamoja na Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanslaus Mabula, wameyapongeza matembezi hayo na kusema kuwa ni ya kizalendo ambapo wamemuomba Katibu Mkuu Mpya, Mhandisi John Kijazi kuhakikisha ahadi aliyoiacha Sefue inatimia ili msanii Rich4D afanikiwe kuonana na rais magufuli.
Staa Fid Q
Msanii Rich4D anaechipukia kwa kasi Jijini Mwanza ambapo tayari anatamba na ngoma mbili ambazo ni "Tawile" na "Huniwezi".