MANYARA YAPITISHA BAJETI YAKE

mkuu wa mkoa wa Manyara Joel Bendera


Na Woinde Shizza,manyara

Mkoa wa Manyara unatarajia kutumia sh202.1  bilioni kwa ajili ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017, ambapo mishahara itakuwa ni sh5.5 bilioni, matumizi ya kawaida sh2.1 bilioni na sh2.7 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 


Katika mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 mkoa umekadiriwa kukusanya mapato ya ndani ya sh18 bilioni ambapo sh17.9 bilioni ni kwa ajili ya serikali za mitaa na sh192 milioni ni za sekretarieti ya mkoa.


Akisoma mpango wa bajeti ya mkoa huo juzi, Katibu Tawala wa mkoa huo Eliakim Maswi alisema kijiografia Manyara yenye kilomita za mraba 50,921 ni kubwa kuliko baadhi ya mikoa, hivyo inahitaji gharama kubwa za uendeshaji.  


Maswi alisema katika mpango huo wa bajeti, Babati mjini wanatarajia kutumia sh25 bilioni, Babati vijijini sh37 bilioni, Hanang’ sh33 bilioni, Kiteto sh30 bilioni, Mbulu vijijini sh38 bilioni, Mbulu mjini sh6 bilioni na Simanjiro sh19 bilioni.


“Pia tunakabiliwa na changamoto ya kuchelewa au kutopatikana kwa fedha za ruzuku za matumizi ya kawaida na ruzuku ya miradi ya maendeleo, ufinyu wa bajeti wa kuboresha na kujenga miundombinu ya zahanati na shule,” alisema.


Alisema umbali kutoka makao makuu ya halmashauri ya wilaya hadi makao makuu ya mkoa ambapo ni lazima upitie wilaya nyingine kama Kondoa, Monduli na Arusha ili ufike mkoani wakati wa kufuata huduma mkoani pia ni kikwazo.


Hata hivyo, mkuu wa mkoa huo Dk Joel Bendera alizitaka halmashauri zote saba kuhakikisha zinachangia bajeti zao kwa asilimia 60 ya mapato ya vyanzo vya ndani kama serikali kuu ilivyoagiza ili kutekeleza miradi ya maendeleo yao.


“Nitakuwa mkali katika kuhakikisha hilo linatekelezeka hivyo kila halmashauri ihakikishe inakusanya mapato yao na kufikia asilimia 60 kwani mimi ndiye ninayekwenda kuomba kupitishwa kwa bajeti yetu,” alisema Dk Bendera.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post