MBUNGE
wa Ilemela, Angelina Mabula ametoa wito kwa wakazi wa jiji la Mwanza na
maeneo ya karibu kujitokeza kwa wingi kwa sababu ya unyeti wa Tamasha
la Pasaka linalotarajia kufanyika Machi 27 kwenye uwanja wa CCM Kirumba
jijini Mwanza.
Akizungumza jana, Mabula alisema Tamasha la
Pasaka ni la Watanzania wote, lakini mwaka huu wamepata bahati ya
kufikiwa na ujumbe wa neno la Mungu ambao utakemea maovu kama mauaji ya
vikongwe na walemavu wa ngozi 'albino'.
"Binaadam anatakiwa
kubaki na heshima yake, kwani hakuna maisha bora ambayo yanatokana na
kuwaua na kuwakata viungo wenzao, si ubinaadam kabisa tunatakiwa
tumrudie Mungu kwani ndio kimbilio," alisema Mabula.
Mabula
alisema Tamasha la Pasaka limebeba ujumbe wa neno la Mungu hivyo ni
nafasi kwa wakazi wa Ilemela na maeneo ya jirani na hata mikoa mingine
kujitokeza kwa wingi kufanikisha tamasha hilo.
Aidha Mabula
alisema thamani ya Tamasha la Pasaka ni kubwa hivyo Watanzania ni nafasi
yetu Watanzania kumfikishia Mungu sala zetu.
Naye Mwenyekiti
wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama alisema
maandalizi ya kuelekea tamasha hilo yanaendelea vizuri, hivyo wakazi wa
mikoa ya Kanda ya Ziwa wakae mkao wa kula.
Msama alisema
Tamasha la Pasaka litaanza Machi 26 mkoani Geita na kufuatiwa jijini
Mwanza Machi 27 na kumalizia Machi 28 mjini Kahama kwenye uwanja wa
Taifa mkoani Shinyanga.
Msama alitaja viingilio katika tamasha
hilo ni shilingi 5000 kwa wakubwa na watoto shilingi 2000, naye alitumia
fursa hiyo kuwaomba wakazi wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi
kuimuimbia na kumtukuza Mungu.