BREAKING NEWS

Tuesday, September 6, 2011

IMEELEZWA kuwa wanawake wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini nchini ili kujinyanyua kiuchumi kwani wana haki ya kufanya hivyo kuliko kunyong’onyeshwa na mfumo dume uliopo nchini. Hayo yamesemwa na Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Haki Madini la mjini Arusha,David Ntiruka kwenye mafunzo ya ukatili dhidi ya mwanamke na kutambua haki zao za kiuchumi yaliyofanyika jana mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara. Ntiruka alisema lengo la mafunzo hayo yaliyowashirikisha washiriki 20 wa mji mdogo wa Mirerani na kata ya Naisinyai ni kuendeleza juhudi za asasi hiyo za kupiga vita unyanyasaji wowote wa wanawake uliopo kwenye sekta ya madini. “Haki madini ni asasi ya kutetea haki za binadamu hivyo kupitia mafunzo haya washiriki wote na hasa wanawake watatambua na kuelewa haki zao za msingi ikiwemo haki ya kufanya biashara kwenye migodi,” alisema Ntiruka. Alisema baadhi ya viongozi wa machimbo ya madini wanawazuia wanawake kupata maeneo ya kuchimba madini,kufanya kazi kwenye migodi na kufanya biashara machimboni wakati ni haki yao ya msingi. Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuyaelewa na kuyashika mafunzo hayo ili faida ya mafunzo hayo ionekane na pia mafunzo hayo yatawawezesha kuwa na ufahamu wa haki zao. Naye mmoja kati ya washiriki wa mafunzo hayo,Monica Tarimo alisema mafunzo hayo yamewawezesha kutambua mambo mengi ya msingi ikiwemo haki ya mwanamke kuweza kushiriki katika uchimbaji wa madini. Tarimo alisema baadhi ya wanawake hasa waliopo vijijini wanashindwa kudai haki zao kutokana na kutojiamini au kutojua haki zao za msingi hivyo kuendelea kunyanyaswa hivyo kupitia Haki Madini wameweza kutambua mengi.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates